1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo adui kesho rafiki?

Aboubakary Jumaa Liongo13 Machi 2009

Maoni ya wanasiasa wa Ujerumani yanatofautiana kuhusu pendekezo la kuzungumza na Wataliban wenye misimamo ya wastani lililotolewa na Rais wa Marekani Barack Obama

https://p.dw.com/p/HBQW
Mpiganaji wa Taliban akiwa na silaha nzitoPicha: Faridullah Khan

.Kwa maoni ya Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje Gernot Erler wa chama cha SPD,kuzungumza hatima ya Afghanistan pamoja na Wataliban wenye misimamo ya wastani,ni hatua muhimu ikiwa siasa za nchi hiyo zitazingatiwa kwa dhati.Lakini Wataliban wenye misimamo ya wastani ni nani?

Kwa maoni ya Rais Barack Obama huenda ikawa bora kuzungumza na Wataliban wenye misimamo ya wastani.Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ameshauri kuondosha vikwazo vya kutokuwa na uhusiano wo wote ule na kundi la Hezbollah nchini Lebanon. Vile vile kuna dalili za kuregezwa msimamo wa kususia kundi la Kipalestina,Hamas.Nchi za magharibi zipo tayari kubadili misimamo yao kuhusu makundi yaliyoitwa magaidi na kutengwa hadi hivi.


Ingawa sababu za msimamo huo mpya ni tofauti kuhusu makundi hayo matatu,asili yake ni moja.Kwani mtu anaposhindwa kutekeleza lengo lililoazimiwa basi lengo hilo linahitaji kupangwa upya.Na katika mifano yote mitatu,vyama huru vya kisiasa havikufanikiwa kuyaondosha na kuchukua nafasi za makundi hayo ya Kiislamu.Badala yake,makundi hayo katika miaka ya hivi karibuni yamezidi kuimarika.

Nchini Afghanistan Wataliban wanasonga mbele hadi Marekani kuwa na mashaka iwapo kweli wataweza kushinda vita hivyo. Huko Libanon kufuatia vita vya Israel vya mwaka 2006 kundi la Hezbollah limeimarika na limerejea serikalini sawa na kundi la Kipalestina Hamas.

Rais wa zamani wa Marekani George W.Bush alijirahisishia mambo.Kwa maoni yake asieunga mkono upande mmoja basi yupo upande wa pili.Asie na wema yupo na waovu.Lakini sasa Rais Barack Obama anataka kufungua ukurasa mpya.Na baadhi ya wanasiasa katika nchi za Magharibi wamefurahia ishara hiyo mpya kutoka Ikulu ya Marekani.Yaani mtu hana budi kuzungumza na makundi hayo ikiwa hayawezi kushindwa.Lakini hapo kuna hatari ya kusaliti maadili yaliyowapeleka vitani Afghanistan au kushighulikia Mashariki ya Kati.Ghafula kumegunduliwa neno "Wataliban wenye misimamo ya wastani" ili kutuliza dhamiri zao.

Bila shaka wapo wafuasi wa zamani wa Taliban na Hizbollah wanaoweza kushiriki katika mazungumzo na hao wasikataliwe kwa sababu ya kufuata itikadi kali za Kiislamu.Kilicho muhimu ni kuwa wanaheshimu misingi inayotambuliwa kimataifa.


Mwandishi: Philipp/Martin

Mhariri: Othman