1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni leo msema kesho ni muongo Wakenya wamchagua rais mpya

Josephat Charo27 Desemba 2007

Kinyang´anyiro kikali ni kati ya Raila Odinga wa chama cha ODM, Mwai Kibaki wa PNU, na Kalonzo Musyoka wa ODM Kenya

https://p.dw.com/p/CgbH
Rais Kibaki ataka kazi iendeleePicha: DW

Wakenya wanapiga kura leo katika uchaguzi uliokumbwa na kampeni za machafuko na huku kukiwa na madai kwamba serikali inapania kuiba kura. Rais Mwai Kibaki mwenye umri wa miaka 76, aliyeung´oa madaraka utawala wa miaka 24 wa rais mstaafu Daniel arap Moi, anakabaliwa na kitisho cha kushindwa licha ya kuimarika kwa uchumi wa Kenya wakati wa utawala wake wa miaka mitano.

Rais Kibaki anajaribu kukabiliana na upinzani mkali katika uchaguzi mkuu unaofanyika leo katika maeneo yote ya uwakilishi bungeni nchini Kenya. Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa wa mashindano makali ambayo hayajawahi kuonekana katika historia ya nchi hiyo. Madai ya rushwa pamoja na vitisho dhidi ya wapigaji kura na machafuko zimekuwa mada mbiu katika kampeni za uchaguzi huku mgombea wa chama cha PNU, rais wa sasa Mwai Kibaki na mgombea wa chama cha ODM, bwana Raila Odinga, wakiapa kumaliza ufisadi ambao umezuia uwekezaji wa kigeni na kuwagharimu Wakenya mamilioni ya dola.

Mapema alfajiri ya leo maelfu ya Wakenya kutoka Pwani hadi mitaa ya madongo poromoka na maeneo ya milimani, wameunga foleni ndefu kupiga kura zao, wengi wao wakilindwa na maafisa wa polisi. Wachambuzi wanasema ni vigumu mno kubashiri mshindi wa uchaguzi huo.

Jana maafisa wa serikali walisema wafuasi wa upinzani waliwapiga mawe maafisa watatu wa polisi mpaka wakafa magharibi mwa Kenya, wakiwashutumu kwa kuwa sehemu ya njama ya serikali kutaka kuiba kura. Grace Kaindi, kamanda wa polisi wa eneo hilo, amesema machafuko yalianza juzi Jumanne wakati maafisa 50 wa polisi walipowasili kwa basi huko Mbita, karibu kilomita 310 magharibi mwa mji mkuu, Nairobi.