1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni miaka 50 tangu kuanzishwa Benki Kuu ya Ujerumani

31 Julai 2007

Noti za mwanzo za sarafu ya Kijerumani, Deutsch Mark, punde baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia zilichapishwa Marekani.

https://p.dw.com/p/CHAE
Jengo la Benki Kuu ya Ujerumani, mjini Frankfurt.
Jengo la Benki Kuu ya Ujerumani, mjini Frankfurt.Picha: AP

Mashirika ya uchapaji hapa Ujerumani mwishoni mwa miaka ya arbaini yalikuwa bado hayana uwezo wa kuchapisha noti hizo. Noti za Deutsch mark zilizochapishwa hapa Ujerumai zilikuja baadae. Na baadae tena ndipo ilipokuja taasisi ambayo ilikuwa ndani ya mfumo wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, nayo ni Benki Kuu ya Ujerumani. Iliundwa July 26, mwaka 1957, na siku chache baadae, hapo Agosti Mosi, ilianza kufanya kazi. Kwa hivyo leo Benki Kuu ya Ujerumani inasheherekea mwaka wa 50 tangu kuanzishwa.

Chini ya noti hizo za mwanzo kulichapishwa vijineno kwa herufu ndogo sana yanayosema hivi: Mtu atakayeghushu au kuengezea kitu juu ya noti hii na kuisambaza ataadhibiwa kwa kupewa kifungo kisichopungua miaka mitano gerezani. Kama kitisho hicho kiliwatia hofu walanguzi, haijulikani. Lakini maneno hayo yalibakia juu ya noti hizo kwa miongo, na kuna sababu nzuri ya kufanya hivyo. Deutsch Mark haijawa tu ni fedha, haijawa tu sarafu kama nyingine- ilikuwa zaidi ya hivyo.

+ Deutsch Mark iliokuwa thabiti ilikuwa msingi muhimu wa utulivu wa jamii iliochipuka chini ya uhuru na demokrasia. Uthabiti wa D-Mark ulisaidia kujenga msingi muhimu wa jamii ya kiraia, kwani bila ya sarafu iliokuwa imara inakuwa vigumu kujenga hali ya kujitegemea na kujichukulia dhamana.+

Hayo ni maneno ya Hans Tietmeyer, mtu aliyewahi kuwa mkuu wa Benki Kuu ya Ujerumani, aliyoyatoa mwaka 1999. Wakati huo D Mark ilikuwa ikisheherekea mwaka wa 50 tangu ianzishwe na alikuwa na fahari juu ya utulivu wa sarafu hiyo iliokuwa imara kabisa. Hali hiyo haijaja kwa urahisi; ilikuja baada ya vita viwili vikuu vya dunia, ughali mkubwa kabisa wa maisha na mfumko wa bei katika miaka ya 20 na baadae kufanywa mabadiliko ya sarafu.

Mashubaka yaliojaa bidhaa madukani yalikuwa ni alama ya kufanikiwa marekebisho ya siasa za uchumi na sarafu. Katika nchi nyingine za Ulaya watu walianza kustaajabishwa na kukuwa haraka kwa uchumi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani na walikuwa waionea wivu.

Ni mwaka 1949 ndipo lilipoundwa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, na nchi zilizoshirikiana kushinda vita hivyo tangu mwanzo ziliweka uzito kuona kwamba sekta ya benki katika Ujerumani pia iwe ya mfumo wa shirikisho. Akilini watu bado walikuwa wanakumbuka madhara yalioachwa na benki kuu, kwa jina la Reichsbank, wakati wa Kaizari.

Benki hiyo ilikuwa inatumiwa kwa kuendesha siasa zenye kuweza kuwekewa alama ya kuuliza, kama vile kutoa mikopo isiokuwa na dhamana ili kugharimia vita. Mwishowe benki hiyo ilikuwa na dhamana ya mauaji ya kiholela na vita vilivoanzishwa wakati wa utawala wa Wanazi.

Benki ya Mikoa ya Ujerumani ilijifunza kutokana na makosa hayo na kutoka mwaka 1951 ilijitangaza kuwa ni huru, yenye kujitegemea yenyewe.

Hali hiyo imebakia vivyo hivyo baada ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani katikati ya miaka ya hamsini kurejeshewa heshima ya utawala wake. Kidogo kidogo kukaanza kuchomoza taasisi mpya, moja yao ni Benki Kuu ya Ujerumani. Jambo hilo lilipitishwa na bunge mwaka 1956. Kansela wa kwanza wa Ujerumani, Konrad Adenauer, alisema yeye angependa angekuwa na ushawishi mkubwa zaidi ndani ya benki hiyo, lakini alitambua kwamba itambidi aishi na benki hiyo katika hali hiyo.

+ Waheshimiwa Mabwana. Benki Kuu ni huru kabisa mbele ya serekali ya Ujerumani. Hapa tuna chombo ambacho hamna aliye na dhamana nacho, sio bunge, pia sio serekali. Kwa fikra zangu ni kwamba ni kubwa zaidi dhamana ambayo kila mtu aliye katika chombo kama hicho ataibeba mwenyewe.+

Rais wa benki hiyo baadae, Karl Klasen, alisema katika miaka ya mwanzo kulikuweo hali ambayo wanasiasa hawajakubaliana na benki hiyo, kama vile kuhusu riba za mikopo, na namna ya kupambana na mripuko wa bei za bidhaa, lengo kubwa la benki hiyo.

Sasa D Mark ni historia. Benki Kuu ya Ujerumani haiamui tena juu ya ukubwa wa riba za mikopo. Sasa watu hapa Ujerumani wanalipa na kulipwa kwa sarafu ya Euro inayosimamiwa na Benki Kuu ya Ulaya. Kuachana na D- Mark ilikuw ani hatua kubwa iliochukuliwa na wajerumani ambao waliuzowea uimara wa sarafu yao ya zamani. Lakini serekali ya Ujerumani, kabla ya Euro kuanza kufanya kazi iliweka masharti mawili; nayo ni kwamba Benki Kuu ya Ulaya iwe huru na isiingiliwe na wanasiasa, wala isipokee maagizo kutoka kwao, na kwamba Benki Kuu ya Ulaya ijishughulishe hasa kuona sarafu hiyo inakuwa imara, na ughali wa maisha na mripuko wa bei unadhibitiwa.