1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watu wa Jamii Asilia

9 Agosti 2012

Siku hii maalum kwa ajili ya kutambua na kulinda haki za jamii hizo ulimwenguni inazongwa na ugunduzi kwamba vyombo vya habari vinachangia katika kuzitenga jamii hizo na maendeleo ya kisasa kwa kuelezea upande mmoja tu.

https://p.dw.com/p/15mCr
Mwanamke wa jamii asilia za Bolivia.
Mwanamke wa jamii asilia za Bolivia.Picha: Sara Shahriari

"Katika siku hii ya kimataifa, ninaomba uungaji wenu mkubwa kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kushirikiana na watu wa jamii asilia, vikiwemo vyombo vyao vya habari, ili kuhakikisha utekelezwaji kamili wa Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusiana na jamii hizo." Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema katika ujumbe wake kwa siku hii.

Kwa mara ya mwazo siku hii ilitangazwa na Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa Disemba mwaka 1994, kwamba ingeliadhimishwa kila mwaka katika Muongo wa Kwanza wa Kimataifa kwa Jamii za Watu Asilia Duniani, ambao ulianza mwaka 1995 hadi 2004. Na baadaye mwaka 2004, Hadhara Kuu ikatangaza mingine kumi ya kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 kuwa Muongo wa Vitendo na Heshima kwa watu wa jamii asilia.

Mada kuu ya maadhimisho ya mwaka huu ni Vyombo Habari vya Asilia Kuziwezesha Sauti Asilia." Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hivi leo kunafanyika mkutano unaozungumzia umuhimu wa vyombo vya habari kupambana na dharau dhidi ya jamii asilia na dhima ya vyombo hivyo katika kuutangaza utambulisho wa jamii hizo, kuwasiliana na ulimwengu wa nje na pia kuhakikisha kuwa jamii za watu asilia zinaweza kuwa na nguvu kwenye ajenda za kijamii, kiuchumi na kisiasa katika mataifa yao.

Dharau za Vyombo vya Habari

Miongoni mwa dharau ambazo zinatakiwa kuvunjwa na vyombo vya habari ni ile ya kuhusisha ajenda nzima ya jamii za watu wa jamii asilia na ngoma, matambiko, mizimu au wafu tu. Katika hili, picha imejengwa kama kwamba jamii za watu asilia ni zile zisizoweza kubadilika na wakati wala kuendana na mahitaji ya sasa kilimwengu.

Jamii ya watu asilia ya Brazil.
Jamii ya watu asilia ya Brazil.Picha: dapd

Hili, anasema Duncan McCue, kwamba linapaswa kupigwa vita na vyombo vyenyewe vya habari. McCue mwenyewe ni wa asili ya jamii ya Chippewas wa Kisiwa cha Georgina kusini mwa mji wa Ontario, Canada, na amekuwa akilifanyia kazi Shirika la Utanganzaji la nchi hiyo tangu mwaka 1998.

Akiwa profesa katika Chuo Kikuu cha British Columbia, mwaka jana McCue alianzisha kozi ya uandishi wa habari inayoitwa Kuripoti katika Jamii Asilia, na pia mtandao unaotoea maelezo ya namna ya kuripoti masuala ya jamii hizo.

Alichogundua McCue hadi sasa ni kwamba mtu wa jamii asilimia anaweza tu kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari kama amefanya yale anayoonekana kuwa ndio maisha yake, yaani kupiga na kucheza ngoma, kuabudu mizimu, kufanya matambiko na kuvaa mavazi ya ngozi, manyoya na au rubega.

Kwa ufupi ni kuwa jamii za watu asilia hazipatiwi nafasi inayostahiki kwenye vyombo vya habari, na wanapopatiwa ni ile inayowaweka kwenye kundi lile lile kila siku na kila saa. Katika jamii za Afrika ya Mashariki kwa mfano, kila siku Mmaasai akiwasilishwa kwenye vyombo vya habari, ni kama Morani, mchungaji ng'ombe na mcheza ngoma ya kuruka na mshale.

Hivi leo ambapo ulimwengu una zaidi ya watu milioni 370 wanaoaminiwa kuwa wa jamii asilia, vyombo va habari vina jukumu kubwa na la pekee kuhakikisha kuwa sauti za kweli za watu hao zinapata nafasi ya kusikika, hadithi za maisha yao kuelezwa na wenyewe kuwa sehemu ya kuunda ajenda zinazohusu maisha yao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/IPS/Umoja wa Mataifa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman