1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni Siku ya Wafanyakazi Duniani

1 Mei 2015

Leo ni Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambapo wafanyakazi duniani kote wanaungana na wenzao kuadhimisha siku hii, huku kinachoangaziwa zaidi kwa mwaka huu wa 2015 kikiwa ni 'mazingira salama na mazuri kwa afya kazini'.

https://p.dw.com/p/1FIgG
Wafanyakazi wakiandamana Taiwan, kudai nyongeza ya mishahara
Wafanyakazi wakiandamana Taiwan, kudai nyongeza ya mishaharaPicha: dapd

Shirika la Kazi Duniani-ILO, limetoa wito siku ya wafanyakazi duniani kwa mwaka huu kuzingatia zaidi usalama na afya kazini na hali hiyo inapaswa kuheshimiwa kwa wafanyakazi wa ngazi zote.

Kwa mujibu wa ILO, serikali, waajiri pamoja na wafanyakazi wanatakiwa kushiriki katika kuhakikisha mazingira ya kufanyia kazi ni salama kwa afya ya wafanyakazi, mfumo ambao utaelezea haki, majukumu na wajibu, ambapo kipaumbele kikubwa kikiwa kuhakikisha kuna mazingira mazuri.

Siku hii leo inaadhimishwa kwa maandamano, ambapo viongozi wa mataifa wamekuwa wakitoa hutuba zao kuzungumzia masuala mbalimbali yakiwemo yanayohusu maslahi ya wafanyakazi.

Mjini Berlin, Ujerumani, kiasi watu 200,000 wanatarajiwa kushiriki katika maandamano yaliyoandaliwa na mashirika ya wafanyakazi yanayofuata mrengo wa kushoto, huku kukiwa na ulinzi mkubwa wa polisi.

Aidha, polisi mjini Istanbul, Uturuki wako katika tahadhari, baada ya serikali kuonya kuhusu uchochezi wowote utakaofanywa, huku serikali ikiufunga uwanja muhimu wa Taksim kuwazuia waandamanaji.

Maandamano ya kudai haki za wafanyakazi

Kwa upande wa Urusi, vyama vya wafanyakazi vitakutana kwenye uwanja Mwekundu mjini Moscow, sambamba na maandamano mengine yaliyoandaliwa na Chama cha Kikomunisti ambapo wafuasi wake watakutana katikati ya mji wa Moscow.

Nembo ya Shirika la Kazi Duniani-ILO
Nembo ya Shirika la Kazi Duniani-ILOPicha: AP GraphicsBank

Nchini Afrika Kusini ambako hivi karibuni kulikuwa na vurugu zinazofanywa dhidi ya raia wa kigeni na kusababisha watu 6 kuuawa, vyama vya wafanyakazi vitafanya maandamano nchi nzima katika kuiadhimisha siku huu.

Ama kwa upande mwingine wafanyakazi barani Asia wameandamana kupinga mageuzi ya ajira yaliyofanywa na serikali. Korea Kusini, wafanyakazi wameandamana wakiapa kufanya mgomo wa nchi nzima iwapo serikali itaendelea kushinikiza mipango yake ya kufanya mageuzi ya ajira. Serikali ya kihafidhina ya Rais Park Geun-Hye inapanga kufanya mageuzi yatakayolihusu soko la ajira, ikiwemo urahisi wa kuwaajiri na kuwafukuza kazi wafanyakazi.

Huko Taiwan, wafanyakazi walirusha mabomu ya kutoa machozi karibu na ofisi ya rais, wakimtaka atekeleze ahadi yake ya kuongeza mishahara pamoja na kulitafutia ufumbuzi suala la ukosefu wa ajira.

Nako Hong Kong wafanyakazi wa nyumbani nao wameandamana wakidai nyongeza ya mishahara pamoja na mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa wafanyakazi ambao ni raia pamoja na wahamiaji.

Siku ya Wafanyakazi Duniani ilianzishwa mwaka 1886 kwa lengo la kumaliza mapambano pamoja na kuhimiza umuhimu wa muda wa saa nane wa kazi kwa siku. Awali mazingira ya kufanyika kazi yalikuwa magumu na watu walifanya kazi kwa muda wa saa 10 hadi 16 kwa siku.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,ILO
Mhariri: Yusuf Saumu