1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni Ujerumani na Austria katika EURO 2008

Kalyango Siraj16 Juni 2008

Kansela Angela Merkel kuhudhuria pambano hilo

https://p.dw.com/p/EKSf
Kocha wa Ujerumani Joachim Loew wakati wa mechi kati ya Croatia dhidi ya Ujerumani .Leo ana kibarua kigumu dhidi ya AustriaPicha: picture alliance/dpa

Mashindano ya soka ya kombe la Ulaya ya mwaka huu baado yanaendelea na mechi kadhaa zilichezwa mwishoni mwa juma.

Uturuki ilifuzu kuingia katika robo fainali baada ya kuikandika Jamhuri ya Czech mabao matatu kwa mawili.

Utamu wa mechi hiyo ni kuwa Uturiki ilipata ushindi huo kwa kufunga mabao matatu kwa kipindi cha dakika 15 kabla ya mechi kumalizika.Kabla ya hapo ilikuwa imefungwa mabao mawili bila jibu.Tena Uturuki ilikuwa inatumia watu 10 tu baada ya mlinda lango wake Volkan Demirel kupewa kadi nyekundu baada ya kumchezea visivyo mshambulaiji wa Czech Jan Koller ambae ni mojawapo wa wachezaji waliofunga bao kupitia hedi safi.Sasa Uturuki inasubiri kukutana na Croatia.

Mechi nyingine iliosisimua kutokana na matokeo ni kati ya Ureno ambayo tayari imefuzu kwa robo fainali dhidi ya wenyeji Uswisi ambao tayari wameshaondolewa.

Hata hivyo Uswisi iliweza kushinda mechi yake ya mwisho kwa mabao 2 kwa bila. Mabao yote yalifungwa na Yakin. Hiyo ndiyo mechi pekee ya Uswisi walioshinda katika mashindano haya.

Na leo jumatatu kuna kivumbi na jasho katika kundi B ambapo mabingwa wa kombe hilo mara tatu Ujerumani watakapo kutana dhidi ya wenyeji Austria.

Ujerumani inahitaji tu sare ili kuweza kujiunga na timu zingine.

Mechi ya leo ni muhimu kwa Ujerumani na inasemekana Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel anatarajiwa kuhudhuria mwenyewe ili kuwapa motisha vijana wake waweze kupata matokeo wanayohitaji ili kusonga mbele la sivyo mambo yao yatakuwa kwisha.

Timu zingine katika kundi hilo B ni Croatia ambaya nayo inacheza dhidi ya Poland.

Mechi kati ya Ujerumani na Austria ina leta hisia za pambano la kombe la dunia la mwaka wa 1978 ambapo Austria iliishangaza Ujerumani ya Magharibi ya wakati huo, ilipoishinda mabao matatu kwa mawili nchini Argentina.

Kuna wanaosema kuwa historia hujirudia,wakisema kuwa Austria ambayo katika orodha ya kimataifa inashika nafasi ya 92 inaweza ikaipiku timu ambayo ni ya tano.

Ikumbukwe kuwa Ujerumani inahitaji tu sare kuweza kusonga mbele.

Habari za kusikitisha kwa Austria ni kuwa hata wakiwashtua tena wajerumani katika mechi ya leo,hilo halitatosha,kwani matokeo ya mechi nyingine, kati ya Poland na Croatia, nayo yanaumuhimu wake.

Yaani Poland yaweza ikabahatika ikapata ushindi wa mabao mengi na wakati huohuo Austria,ikiwa imeshinda,kwa matokeo madogo,hivyo nafasi yake ya kusonga mbele ikiwa imegonga mwamba.

Lakini kama wasemavyo, mchezea kwao hutunzwa huenda ikawa hivyo,japo filimbi ya mwisho ndio itaamua.

Kesho jumanne kuna ngoma nyingine katika kundi C,ambapo Uholanzi itacheza dhidi ya Romania.

Pia pambano lingine la kesho, kati ya Ufaransa na Italy, huenda likawa marudio ya fainali ya kombe la dunia ya mwaka wa 2006. Italy iliishinda Ufaransa kuweza kutwa kombe hilo.

Swali ni je Ufaransa itakubali kushindwa kama wakati huo na pia je Italy itaweza kurudia wembe uleule kuweza kuwapiku wapinzani wao.Hilo litajulikana hapo jumanne.

Lakini muhimu kwa leo ni mechi kati ya wenyeji Austria dhidi ya wageni Ujerumani.