1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo siku ya kimataifa ya kupambana na rushwa .

Abdu Said Mtullya9 Desemba 2010

Leo ni siku ya kupambana na ufisadi duniani ouvu unaosababisha umasikini hasa barani Afrika.

https://p.dw.com/p/QTwU
Rushwa ni maradhi yanayolemaza jamii!Picha: picture-alliance/dpa

Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na vitendo vya ufisadi na rushwa ulimwenguni.Kauli mbiu ni kukataa kushiriki katika vitendo vyote vinavyoupa nguvu ufisadi kwa minajili ya kupambana na umasikini.Siku hii inaadhimishwa wakati ambapo maafisa wa ngazi za juu wanaosimamia vita dhidi ya tatizo hilo wanakutana kwa mara ya kwanza katika majengo ya Benki ya Dunia ili kuvipa msukumo .Kikao hicho kinawaleta pamoja wawakilishi kutoka mataifa 134.

Maafisa wa ngazi za juu wanaohusika na harakati za kupambana na vitendo vya ufisadi na rushwa wanakutana mjini Washington kwa minajili ya kuziongezea kasi hususan katika mataifa masikini.Hii ni mara ya kwanza kiasi ya zaidi ya maafisa 200 wanakutana chini ya mwamvuli wa wanaharakati wa kimataifa wa kupambana na rushwa.Kulingana na Rais wa Benki ya Dunia,Robert Zoellick,mitandao midogo pamoja na juhudi za binafsi vyote vimechangia katika vita hivyo vinavyofanikiwa ila hatua zaidi za pamoja zinahitajika kuchukuliwa.

Katika ufunguzi rasmi wa mkutano huo,Robert Zoellick alifafanua kuwa kuna umuhimu wa kuihakikishia jamii ya wafadhili kuwa kila sarafu wanayoitoa kuchangia katika miradi ya maendeleo itatumiwa kama ilivyonuiwa ili kupambana na umasikini vilevile kuziimarisha juhudi za kuukuza uchumi.

Aliusisitizia umuhimu wa kushirikiana kwa minajili ya kuwasaka wahalifu wanaohusika na vitendo vya rushwa na ufisadi kinyume na malengo yaliyowekwa.

Hii ni mara ya kwanza maafisa hao wanakutana ili kuzijadili mbinu za kufanya uchunguzi wa uhalifu huo vilevile kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wakiwemo wanaoikawamisha miradi ya benki ya dunia.

Kikao hicho cha siku tatu kinafadhiliwa na serikali za Australia,Norway na Denmark.Kulingana na kiongozi huyo wa Benki ya Dunia,mafisadi wanawaibia walio masikini ila ni wasiojali wanaowawezesha kuendelea na uhalifu huo.Hata hivyo juhudi za binafsi za kupambana na rushwa zinafaa ila mafanikio yake si makubwa wala kuwa mfumo endelevu wa kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi.Wito huo umeungwa mkono na Ufaransa ambayo mahakama yake kuu,hivi karibuni ililipa idhini shirika la uangalizi wa visa vya ufisadi na rushwa Transparency International,kuchunguza jinsi viongozi watatu wa bara la Afrika walivyojipatia mali yao nchini humo.Hii ni mara ya kwanza kwa hatua kama hiyo kuchukuliwa na shirika lisilo la kiserikali baada ya serikali ya Ufaransa kuutambua mchango wake mbele ya mahakama.

Wakati huohuo,jaji mmoja nchini Msumbiji amewahukumu maafisa wawili wa serikali wa zamani kifungo cha miaka 12 jela kwa kuhusika na wizi wa kiasi ya dola laki moja na tatu,fedha za serikali.

Kulingana na jaji huyo,mmoja wa maafisa hao walizitumia fedha hizo kugharamia safari zilizowapeleka hadi Afrika Kusini na Swaziland,kulipia karo za shule vilevile katika shughuli za starehe za kifahari nchini mwao.Jaji huyo alifafanua kuwa maafisa hao walizivuruga makusudi data za serikali za uhasibu jambo lililoifanya mishahara ya wafanyakazi kucheleweshwa kulipwa.

Kiongozi wa taasisi hiyo wa zamani Orlando Come na mwenzake wa taasisi ya uratibu na fedha Manuel Vilanculos walitakiwa kuzilipa fedha hizo walizoziiba.

Kulingana na tathmini ya Shirika la uangalizi,Transparency International,Msumbiji ni ya moja kati ya nchi 50 zilizo na vitendo vingi zaidi vya rushwa na ufisadi kote ulimwenguni.Ripoti kamili ya tathmini ya hali ya nchi ulimwenguni katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi itachapishwa baadaye hii leo.

Mwandishi: Mwadzaya,Thelma-AFPE/APE

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed