1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo tarehe 21 Machi ni siku ya kimataifa dhidi ya ubaguzi.

Mohammed Abdul-Rahman20 Machi 2007

Katika masuala ya haki za binaadamu kinachosimama usoni kabisa ni haki na usawa kwa kila binaadamu.

https://p.dw.com/p/CB5A

Ubaguzi si jambo geni, kwani umekuweko wakati wa ukoloni barani ulaya na hata wakati wa enzi ya biashara ya utumwa , walipovushwa na kupelekwa bara la Amerika.

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa anayehusika na ubaguzi Doudou Diéne, alionya mnamo miezi ya nyuma juu ya hali ya ubaguzi katika jamii ya magharibi,akitaja juu ya udhaifu wa mkakati wa kisiasa na sheria katika vita dhidi ya ubaguzi katika nchi husika. Kwa mfano akizungumzia kuhusu umuhimu wa kulishughulikia tatizo hilo, anatoa mfano wa marekani na kitabu kilichoandikwa na mwandishi mmoja Samuel Hutington.anasema ,“Kitabu cha mwisho cha Samuel Hutington kinaitwa“Sisi ni Nani," -ufafanuzi juu ya suala la nani hasa Mmarekani.

Katika kitabu hicho anataja juu jamii ya walatino, kuwepo kwao na utamaduni wao. Anaonyesha kwamba kuwepo kwao ni kitisho kwa wamarekani. Sasa unapokua na mhadhiri anayesomesha katika chuo maarufu kama HAVARD akikuza fikra na mtazamo kama huo, kwa kweli ni jambo linalomshitua kila mtu na ina maana tunarudi katika jambo ambalo ni kubwa na la hatari.“

Kongamano la kimataifa dhidi ya ubaguzi lililofanyika katika mji wa bandari wa Durban nchini Afrika kusini 2001, lilisisitiza kwamba ili kupambana na ubaguzi ambalo limegeuka tatizo la dunia nzima, panahitajika mpango wa kivitendo wa pamoja duniani.

Petra Follmar Otto kutoka taasisi ya haki za binaadamu mjini Berlin. Akizungumzia hali katika Ujerumani anasema,“Kwa kuzungumzia chuki dhidi ya wageni maana yake tayari ni kwamba watu wanaobaguliwa ni wageni.

Lakini mara nyingi sivyo. Wengine wana pasi za kusafiria za Ujerumani au wazazi wao tayari wana pasi za kusafiria za hapa. Huenda familia zao ziomeshaishi Ujerumani kwa muda mrefu, lakini kutokana na kuwa na sura tafauti, rangi za ngozi au jina la lugha nyengine, bado wanaangaliwa kama wageni.“

Wengi miongoni mwa wanaadamu na hata nchini Ujerumani pia wanabaguliwa sio tu kwa kuwa ni wahamiaji wenye utamaduni tafauti, bali kuna ubaguzi wa aina nyengine kwa mfano katika kupata nyumba au ajira, lugha au hata katika viwanja vya kandanda.

Ilikaua vigumu kwa bunge la Ujerumani kukubaliana juu ya kujumuisha sheria ya umoja wa ulaya dhidi ya ubaguzi katika sheria ya taifa, lakini hata hivyo bado kuna mkakati wa kitaifa kupiga vita ubaguzi, kama ilivyotakiwa katika mkutano wa umoja wa mataifa mjini Durban.

Ubaguzi ni tatizo la dunia nzima. Katika bara la Afrika ambako miaka ya karibuni imeshuhudia vita katika nchi kadhaa barani humo, chanzo cha baadhi ya migogoro ni tafauti za kikabila. Huko Zimbabwe kwa mfano kumekuweko na hisia za kibaguzi dhidi ya wakulima wakizungu kutokana na umasikini na ukosefu wa ardhi kwa waafrika walio wengi.

Hadi karibuni Afrika kusini iligeuka mhanga wa ubaguzi wa wachache dhidi ya walio wengi. Ubaguzi unakutikana pia Asia na Mashariki ya kati. Siku ya leo ya kimataifa ya kuupiga vita ubaguzi kwa hivyo, inakumbusha juu ya haja ya kutekelezwa mpango wa hatua za pamoja za kimataifa kama ilivyopendekezwa katika kongamano la kimataifa mjini Durban miaka 6 iliopita.