1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lesotho: Naibu waziri achukua hatamu

Admin.WagnerD1 Septemba 2014

Waziri Mkuu wa Lesotho Thomas Thabane ambaye amekimbilia Afrika Kusini kuepuka kile anachokitaja kuwa mapinduzi ya kijeshi dhidi yake, amemshutumu naibu wake kupanga njama ya kumuondoa madarakani.

https://p.dw.com/p/1D4hW
Wanajeshi wa Lesotho ambao wanashutumiwa kumpindua waziri mkuu
Wanajeshi wa Lesotho ambao wanashutumiwa kumpindua waziri mkuuPicha: picture-alliance/AP Photo

Naibu waziri mkuu huyo Mothetjoa Metsing kwa sasa amechukua madaraka ya kuiongoza nchi baada ya Thabane kukimbia mwishoni mwa Juma. Kufuatia ''mapinduz''i hayo ya kijeshi nchini Lesotho siku ya Jumamosi, rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ambaye ni mwenyekiti ya kitengo cha siasa cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC, usiku wa leo amefanya mazungumzo na mawaziri wa ulinzi na mambo ya nchi za nje kutoka wa Zimbabwe na Namibia. Mkutano huo umefanyika nchini Afrika Kusini.

Waziri Mkuu wa Lesotho Thomas Thabane aliwasili Afrika Kusini Jumamosi, akikimbia kile alichokitaja kuwa njama za kijeshi kuipindua serikali yake. Kiongozi huyo ambaye alitoroka kabla ya wanajeshi kuwasili nyumbani kwake, amemshutumu naibu wake Mothejoa Metsing ambaye ni mshirika katika mseto wa vyama vinavyoiongoza nchi hiyo, kuwa mpangaji wa njama hiyo ya mapinduzi, ambayo amesema hayatafanikiwa.

Thomas Thabane, waziri mkuu wa Lesotho ambaye anasema zimekuwepo njama za kumpindua
Thomas Thabane, waziri mkuu wa Lesotho ambaye anasema zimekuwepo njama za kumpinduaPicha: picture-alliance/dpa

''Tuhuma juu ya njama ya mapinduzi ilikuwa na msingi. Ulikuwepo mpango wa kufanya mapinduzi lakini umewahiwa na kuzuiliwa. Tunafanya juhudi kurejesha hali ya kawaida haraka iwezekanavyo''. Amesema Thabane.

Jeshi lakanusha tuhuma

Hata jeshi la Lesotho limekanusha shutuma kwamba limempindua waziri mkuu. Msemaji wake Kapteni Ntlele Ntoi, amesema jeshi liliingilia kati katika kituo cha polisi, baada ya kung'amua kwamba polisi ilikuwa ikipanga kukipa silaha chama cha waziri mkuu cha All Basotho Convention ili kiweze kuvunja maandamano yaliyopangwa na chama cha naibu waziri mkuu cha Lesotho Congress for Democracy.

Amesema, ''Suala hili la kila mara kuibuka na shutuma kwamba jeshi la ulinzi la Lesotho linapanga mapinduzi ni tuhuma zisizo na msingi wowote''.

Metsing aziba pengo

Wakati haya yakijiri, naibu waziri mkuu Mothetjoa Metsing amechukua hatamu za uongozi wa nchi. Waziri wa mawasiliano, sayansi na teknolojia wa Lesotho Selibe Mochoboroane ambaye pia ni msemaji wa chama cha Metsing, amesema kwa mujibu wa katiba ya nchi, ikiwa waziri mkuu hayuko nchini, majukumu ya uongozi humuangukia naibu wake.

Lesotho ni nchi ndogo iliyozingirwa pande zote na Afrika Kusini
Lesotho ni nchi ndogo iliyozingirwa pande zote na Afrika Kusini

Msemaji huyo ambaye pia ameunga mkono kauli ya jeshi kwamba hakuna mapinduzi yaliyotokea, amesema naibu waziri mkuu huyo amealikwa kwenye mazungumzo nchini Afrika Kusini, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu wengine watakaoshiriki katika mazungumzo hayo.

Uhusiano kati ya waziri mkuu na naibu wake, ambao vyama vyao vimeunda ushirika unaoiongoza nchi, umevurugika mnamo siku za hivi karibuni. Waziri Mkuu Thomas Thabane alilivunja bunge mwezi June kuepuka kura ya kutokuwa na imani naye, hali ambayo ilimfanya naibu wake Mothetjoa Metsing kutangaza nia ya kuunda ushirika mwingine ambao ungemtimua madarakani waziri mkuu.

Jana, Umoja wa Afrika ulitangaza kwamba kamwe hautavumilia unyakuaji wa madaraka kwa njia zisizo halali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe/Africalink

Mhariri:Yusuf Saumu