1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya huenda ikashindwa kuandaa uchaguzi

10 Aprili 2012

Vurugu zinazoendelea nchini Libya hivi sasa zinaweza kuuathiri uchaguzi wa Juni 2012 kama serikali itashindwa kuimarisha udhibiti wa kisiasa na kuufanyia marekebisho mfumo wake wa kisheria ambao una mapungufu mengi.

https://p.dw.com/p/14aYg
Mapigano katika mji wa Sabha.
Mapigano katika mji wa Sabha.Picha: Reuters

Katika miji ya jangwa la kusini, Sabha na Kufra, mapigano kati ya watu wa makabila ya Kiarabu na wasio Waarabu yamegharimu maisha ya watu 250 tangu mwezi Februari mwaka huu, kwa mujibu wa hisabu ya shirika la habari la AFP iliyotokana na tathmini rasmi za serikali.

Mapigano ya ndani magharibi mwa LIbya wiki iliyopita yalisababisha vifo vya watu 20 na mamia ya majeruhi, kabla ya serikali kuingilia kati kuitisha usitishaji mapigano kwa msaada wa jeshi na vikosi vya wanamapinduzi.

Machafuko haya yanasindikizwa na wito wa kujitenga kutoka mashariki ya nchi hiyo, ambao umetia shaka uwezo wa Baraza la Mpito la Taifa kuitawala Libya, ambayo inasumbuliwa na ukosefu wa taasisi kufuatia miongo kadhaa ya udikteta.

Vile vile yameuweka uwezo wa Baraza hilo kuendesha uchaguzi wa bunge la katiba hapo mwezi Juni kwenye alama ya kuuliza. Mhariri wa jarida la Masomo ya Kaskazini mwa Afrika, George Joffe, anasema machafuko haya yataendelea na yatakuwa ya mara kwa mara kwa sababu ya kukosekana serikali kuu yenye uwezo.

Vichocheo ni vingi

Na kuna vichocheo vingi tu hadi sasa: hamu ya uhuru mashariki mwa Libya, kisasi baina ya watu au makundi yanayoshukiwa kushirikiana na utawala uliopita, hofu za kikabila, na hamu ya kusalia madarakani, anasema Joffe.

Mpiganaji akibeba silaha yake aina RPG katika mapigano ya kikabila ya Libya.
Mpiganaji akibeba silaha yake aina RPG katika mapigano ya kikabila ya Libya.Picha: Reuters

Joffe ameiambia AFP, kwamba mapigano ya kikabila "yanaweza kukiharibu kipindi cha mpito kuelekea demokrasia kwa kuzuia ufanyikaji wa uchaguzi wenye ufanisi".

Naye Peter Cole wa International Crisis Group anasema kwamba hata kama vyanzo vya migogoro huwa si vya kikabila, lakini "utiifu kwa jamii na makabila una nafasi kubwa sana linapozuka suala la hasira za watu".

Cole amesema kwamba ikiwa serikali haitaweza kuweka mfumo mzuri wa kisheria, ni wazi kuwa migogoro ya kijamii itakuwa na kuongezeka, kwani watu wana tabia ya kuchukuwa sheria mikononi mwao kwa kuwaadhibu wale wanaodhani ni wakosa.

Cole ambaye alikuwa Sabha hivi karibuni, amesema kwamba Libya iko kwenye kilele cha kuporomoka, kwani mabaraza ya upatanishi na viongozi wa kikabila wameshindwa kudhibiti migogoro ya watu binafsi kugeuka kuwa migogoro ya makundi.

Lazima wanamgambo wanyang'anywe silaha

Mshauri maalum wa Shirika la Haki za Binaadamu nchini Libya, Fred Abrahams, anasema serikali ya mpito inahitajika kulichukulia suala la ujenzi wa mfumo mpya wa kisheria kwa umakini mkubwa zaidi.

Wapiganaji wakijitayarisha katika mapigano ya Sabha.
Wapiganaji wakijitayarisha katika mapigano ya Sabha.Picha: Reuters

Miongoni mwa yanayohitajika kufanyika, kwa mujibu wa Abrahams, ni kuyanyang'anya silaha makundi ya wanamgambo na kuwaachia huru wafungwa 8,000 walio kwenye mikono ya wanamgambo hao.

Hii ndio maana haishangazi kwamba wapiganaji wa kikabila wamerukia kujaza ombwe la madaraka lililopo na halikuwa jambo la sadfa kwamba mapigano ya hivi karibuni yalitokea maeneo ya mpakani.

Kwa mujibu wa Abrahams, mapigano hayo mara nyingi ni kuhusu biashara na udhibiti wa njia za kupitishia magendo, ambako kuna fedha nyingi sana kutokana na biashara ya silaha.

Hata hivyo, ikilinganishwa na mapigano ya kwanza ya mwezi Februari katika mkoa wa Kufra, kwa siku za karibuni serikali imejitahidi kuchukuwa hatua kwa wakati. Lakini wachambuzi wanaona kuwanyang'anya silaha wanamgambo ni jambo la kwanza na la muhimu, na ambalo Baraza la Mpito la Libya limeonesha udhaifu wake.

Baraza hilo linakabiliwa na vita vyake vya ndani kwa ndani vya madaraka, upungufu wa rasilimali za kuifanya kazi hiyo na pia ukweli kwamba madaraka yake hayafiki nje ya eneo la mashariki ya Libya lilikozaliwa. Yote haya yanalifanya lionekane "chui wa karatasi."

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman