1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yaijibu ICC

28 Juni 2011

Serikali ya Muammar Gaddafi imeijibu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) baada ya kutoa waranti wa kukamatwa kwa Gaddafi, ikisema kuwa Mahakama hiyo si huru na ni chombo kinachotumiwa na mataifa ya Ulaya.

https://p.dw.com/p/11kfd
Mwendesha mashitaka Mkuu wa ICC Luis Moreno OcampoPicha: picture alliance/dpa

Libya imeukataa waranti uliotolewa na ICC kuwakamata Gaddafi, mwanawe Saif al-Islam na Mkuu wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo, Abdullah al-Senussi, kutokana na tuhuma za kufanya vitendo vya ukatili katika vita vinavyoendelea sasa nchini humo.

Waziri wa Sheria wa Libya, Mohammed al-Gamudi amesema uamuzi huo unatimiza matakwa ya NATO ambao mpaka sasa wanaendelea na jaribio la kutaka kumuuwa Gaddafi.

Gemudi amesema nchi yake haikutia saini mkataba wa Roma kwa hiyo haikubali mamlaka ya mahaka ya kimataifa ya uhalifu ICC.

Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Libya, Khaled Kaaim amesema ICC inafanaya kazi kama chombo cha kutekeleza sera za mambo ya nje ya Ulaya.

Lakini Kiongozi wa Baraza la Mpito la Waasi, Mustafa Jalil aliuambia mkutano wa vyombo vya habari kwamba " haki imetendeka"

London Obama Rede Britisches Parlament
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Mjini washington,Ikulu ya Marekani imesema uamuzi wa ICC unadhirishwa kwamba Gaddafi amepoteza uhalali wa kuongoza jambo ambalo pia limepokewa vyema na Uingereza, kama miongoni mwa nchi zinazoongoza operesheni za kuzuia ndege kuruka nchini Libya na kuwalinda raia wa nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, William Hague ametoa wito kwa watu walio karibu na Gaddafi wamuache mkono.

Akizungumzia hatua hiyo nae, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema suala lililobaki sasa sio kwamba Gaddafi anaweza kuondoka madarakani! bali lini, bali lini atayaacha madaraka.

Katika hali tafauti na misimamo hiyo , Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini ameonesha wasiwasi na kusikitishwa kwake kufuatia uamuzi wa ICC kutoa waranti ya kukamatwa kwa Kanal Gaddafi.

Akizungumza katika redio ya serikali ya Afrika Kusini SABC, msemaji wa rais Zuma, Zizi Kodwa amesema uamuzi huo unafanyika wakati jitihada za upatanishi za jopo la upatanishi la Umoja wa afrika zimepiga hatua.

Mapigano yameendelea leo ambapo wapiganaji waasi wameshambulia ghala moja ya silaha ya majeshi ya Gaddafi lililopo eneo la jangwa, umbali wa kilometa 25 kutoka mji wa Zintan, uliyopo kus/mash mwa mji mkuu- Tripoli.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP

Mhariri; Abdul-Rahman, Mohammed