1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Licha ya hotuba ya Tantawi, Tahriri yaendelea kurindima

23 Novemba 2011

Maelfu ya Wamisri wameendelea kuandamana katika uwanja wa Tahrir wakiutaka utawala wa kijeshi uondoke madarakani, licha ya ahadi iliyotolewa na Baraza la Kijeshi ya kukabidhi madaraka kwa rais atakayechaguliwa mwakani.

https://p.dw.com/p/13FIX
Jemedari Mohamed Hussein Tantawi, Mkuu wa Baraza Kuu la majeshi nchini Misri.Picha: dapd

Kiongozi wa Baraza Kuu la Kijeshi nchini Misri, Jemedari Hussein Tantawi, aliyekuwamo katika Baraza la Mawaziri wakati wa utawala wa Rais Hosni Mubarak ameahidi kuitisha uchaguzi wa Urais hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa Juni mwakani.

Jemedari Tantawi pia amesema kwamba yupo tayari kuyakabidhi mamlaka mara moja, kwa njia ya kupiga kura ya maoni, ikiwa wananchi wa Misri watataka iwe hivyo. Katika hotuba aliyoitoa kwa wananchi, Jemedari Tantawi alisema kuwa jeshi halina dhamira ya kuendelea kayashikilia mamlaka ya kisiasa.

Lakini licha ya kutoa ahadi hiyo ya kukabidhi mamlaka mara moja kwa njia ya kura ya maoni, maalfu kwa maalfu ya Wamisri waliendelea na maandamano kwenye uwanja wa Tahrir mjini Cairo ya kumpinga Jemedari Tantawi mara baada ya habari juu ya tamko lake kuwafikia wananchi. Maalfu ya Wamisri wamesema hawakuamini walichokuwa wanakisikia. Waandamanaji kwenye uwanja wa Tahrir wamesema wanachotaka kukisikia sasa ni kuondoka kwa utawala wa kijeshi nchini Misri.

Mapambano yalizuka tena leo baina ya polisi na wapinzani wa utawala wa kijeshi. Radio ya serikali imearifu kwamba mapambano hayo yalitokea karibu na uwanja wa Tahrir. Polisi wa kuzuia fujo walitumia gesi ya kutoa machozi ili kuwakabili waandamanaji waliokuwa wanawashambulia polisi kwa mawe.

Wakati huo huo gazeti maaruf la al-Ahram limearifu kwamba mtoto mchanga amekufa kutokana na gesi ya kutoa machozi iliyotumiwa na polisi katika kuwakabili waandamanaji katika mji wa Tanta uliopo kwenye bonde la Mto Nile. Mtoto huyo mchanga aliekuwa na umri wa miezi 9 pamoja na mama yake walikuwa karibu na makao makuu ya Baraza la Usalama wakati polisi walipoitumia gesi hiyo ya machozi ili kuwazuia waandamanaji kuingia katika jengo la Baraza hilo.

Kwa mujibu wa taarifa watu wasiopungua 35 wameshakufa tokea jumamosi iliyopita nchini Misri kutokana na hatua za polisi za kuwakabili waandamanaji wanaoupinga utawala wa kijeshi. Hata hivyo taarifa hizo zimetolewa na wahudumu wa afya na mashirika ya kutetea haki za binadamu .Lakini taarifa za serikali zinasema kuwa ni watu 28 tu waliouawa mpaka sasa.

Mwandishi: Abdu Mtullya/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman