1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liemba: Meli kongwe ya Kijerumani katika Ziwa Tanganyika

12 Juni 2011

Kwa karibuni karne nzima sasa, meli ya Kijerumani Graf von Götzen (sasa MS Liemba) imekuwa ikisafiri katika Ziwa Tanganyika ikisafirisha sio watu na mizigo yao, bali pia ikibeba utamaduni na historia pamoja nayo.

https://p.dw.com/p/11XZB
Meli ya Liemba katika Ziwa Tanganyika
Meli ya Liemba katika Ziwa TanganyikaPicha: Simon Collins

Kigoma ni mkoa wa Magharibi ya Tanzania ulio kwenye ufukwe wa upande wa Mashariki wa Ziwa Tanganyika. Meli ya MV Liemba, inayomilikiwa na Shirika la Reli la Tanzania, hung'oa nanga katika mji huu, tayari kwa safari ya kuelekea Mpulungu, Zambia, na baadaye Kassanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ndani ya meli, ni abiria na mizigo yao.

Hakuna anayeweza kusema hasa, ni safari ya ngapi meli hii ya Liemba imeng'oa nanga na kutweka katika bandari hii ya Kigoma. Lakini inafahamika kuwa, hii ni miongoni mwa meli chache duniani kuishi na kuendelea kufanya kazi kwa karibu karne nzima sasa. Hadi mwaka 2015, Liemba itakuwa inatimiza miaka mia moja kamili tangu ianze kuelea kwenye Ziwa Tanganyika, ikiwa imeletwa hapo na Wajerumani mwaka 1915.

Meli ya Liemba

Abiria wakipanda kwenye meli ya Liemba
Abiria wakipanda kwenye meli ya LiembaPicha: picture alliance/Zandbergen-Mc

Kwa mara ya mwanzo, Elisabeth na Franz Hiss, ambao wenyewe ni Wajerumani, walisikia habari za meli hii mwaka 2007, wakiwa Kigoma, ambako walikuwa wakifanya kazi kama washauri wa miradi ya kimaendeleo na Kanisa Katoliki, na hapo hapo mshipa wa mafungamano ya kihistoria kati ya iliyokuwa ikiitwa Deutsche-Ostafrika, yaani koloni la Ujerumani la Afrika ya Mashariki, wakati huo ikiwa Tanganyika, na Ujerumani yenyewe, wanakotokea akina Hiss.

"Mwaka 2007, rafiki yetu aliyeko Ujerumani alituambia kuwa kuna makala kwenye jarida la GEO, ambayo inazungumzia meli ya Liemba. Hii ndiyo makala iliyotuvuta kwenye meli yenyewe na pia kwa kampuni ya Marine Service Company Limited, ambayo inasimamia meli hiyo hivi sasa. Na kwa sababu ya kuiendeleza, tutakutaka na viongozi wa eneo hilo na jumuiya za kimataifa zinazofanya kazi Kigoma, kama vile GTZ, na mkuu wa wilaya, na mkuu wa mkoa na jamii nzima." Anasema Elisabeth Hiss.

Mradi wa "Run Liemba"

Mfano wa meli ya Liemba kwenye Makumbusho ya Hamburg
Mfano wa meli ya Liemba kwenye Makumbusho ya HamburgPicha: cc--sa-2.5-by-WerWil

Hapa ndipo wazo la kuunda jumuiya isiyo ya kiserikali ya Friends of Liemba Foundation (FLF), yaani Wakfu wa Marafiki wa Liemba, lilipoanzishwa. Wakfu huu ambao unawaleta pamoja na Watanzania na Wajerumani, sasa umeanzisha mradi maalumu unaoitwa "Run Liemba".

Mradi huu unataka kuwekeza kiasi ya euro milioni 10, sawa na shilingi bilioni 20 za Tanzania, katika miundombinu inayozunguka eneo la Ziwa Tanganyika. Ziwa hili ni la pili kwa kina cha maji duniani na linaziunganisha nchi nne za Afrika ya Mashariki na Kati: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia.

Miongoni mwa wajumbe wa FLF ni Joseph Bhwana, ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya kampuni inayosimamia meli ya Liemba, Marine Services Company Limited.

Bhwana anasema kuwa mradi huu ni tunu muhimu kwa watu wa Ziwa Tanganyika.

"Mradi huu wa Run Liemba unakusudia kuifanyia matengenezo meli hii na kuinadhifisha ili iweze kuendelea kufanya kazi kwa miaka mingi zaidi.Kwani watu wengi wanaoishi kando kando ya Ziwa Tanganyika wanaishi na kufanya kazi zao za kijamii kwa kutumia Liemba kama njia pekee ya usafiri." Anasema Bhwana.

Historia ya Liemba

Picha ya mwaka 1916 wakati meli ya Liemba ikiwa matengenezoni kwenye Ziwa Tanganyika
Picha ya mwaka 1916 wakati meli ya Liemba ikiwa matengenezoni kwenye Ziwa TanganyikaPicha: cc

Meli ya Liemba ina historia ya kufurahisha. Mwanzoni iliitwa Graf von Götzen, ikipewa jina la gavana wa Kijerumani nchini Tanganyika. Iliamriwa kuletwa kwenye Ziwa Tanganyika na Mfalme Wilhelm wa Pili hapo mwaka 1913.

Ilipewa jina la Liemba, ambalo ni jina la asili ya upande wa Kusini wa Ziwa Tanganyika, na Waingereza katika miaka ya 1920 baada ya kuwashinda Wajerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia, na kuizamua baada ya kuzamishwa kwa makusudi na majeshi ya Ujerumani.

Meli hii iliundwa kwenye kiwanda cha meli cha Meyer-Werft Shipyard, mjini Papenburg, na kisha ikaunduliwa vipande vipande na kusafirikwa kwenye masanduku kutoka bandari ya Hamburg hadi jijini Dar es Salaam, ambao leo ni mji mkubwa wa kibiashara wa Tanzania.

Kutoka Dar es Salaam, masanduku hayo yalibebwa kwa treni hadi karibu na Kigoma, ambako kwa kuwa reli iliishia hapo, yakabebwa kwenye mabega ya watu hadi kwenye Ziwa Tanganyika. Haijulikani ni watu wangapi walifariki njiani wakiwa na shehena na vipande vya MV Liemba mabegani mwao!

Umuhimu wa Liemba

Meli ya Liemba, wakati huo ikijuilikana kama Graf von Götzen, meli ya kivita
Meli ya Liemba, wakati huo ikijuilikana kama Graf von Götzen, meli ya kivitaPicha: picture-alliance/akg-images

Hivi leo, Liemba inafanya safari zake baina bandari ya Kigoma kwa upande wa Tanzania na Mpulungu kwa upande wa Zambia, ikishusha na kupakia abiria na mizigo yao katika vituo kadhaa hapo katikati yake.

Na kama Joseph Bhwana anavyosema, Liemba imekuwa "meli pekee inayowaunganisha watu wanaolizunguka Ziwa Tanganyika na kwa kuwa kwake njia pekee ya usafiri wa uhakika kwenye ziwa hili, mtu anaweza kuuona umuhimu wa meli hii kwa mafungamano ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni ya watu hawa."

Joseph Mbwiliza, aliyewahi kufanya kazi kama mtaalamu kwenye Wakfu wa Mwalimu Nyerere, anasema kwamba Liemba inakwenda mbali zaidi ya kuwa meli ya kusafirisha mizigo na watu tu, bali inatekeleza dhana ya soko la pamoja kwa nchi hizi.

"Tunatarajia sana kwamba Liemba itakuwa kiungo kikubwa cha soko pana la pamoja katika nchi za Mashariki na Kati ya Afrika." Anasema Mbwiliza.

Ni fursa hizi ambazo mradi wa "Run Liemba" unaziona kwamba zinaweza kutumika kuifanya meli hii inayokaribia miaka mia moja, kuishi miaka mingine mia moja ijayo, sio tu kama meli, bali pia kama nyenzo ya mawasiliano, maingiliano na mafungamano ya kijamii, kitamaduni na kijamii.

La mahusiano mema baina ya Tanzania na Ujerumani, likiwa "miongoni mwa yaliyo muhimu sana", kama anavyosema Elisabeth Hiss, mmoja wa waanzilishi wa mradi huu.

"Dhamira ya mradi wa Run Liemba ni kuusaidia Wakfu wa Marafiki wa Liemba kufikia lengo lake. Jukumu letu ni kusaidia kuwepo kwa mashirikiano baina ya Ujerumani na Tanzani kwa kutumia mustakabali wa huduma za meli ya Liemba" Anasema Elisabeth Hiss.

Liemba kama Nyenzo ya Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni

Liemba ikiwa kazini
Liemba ikiwa kaziniPicha: picture alliance/dpa

Lengo hasa ni kuitumia meli ya Liemba kama chanzo cha miradi kadhaa ya kimaendeleo katika eneo la Ziwa Tanganyika, ambamo meli hii imekuwa ikiishi siku nenda-siku rudi.

Miundombinu itajengwa katika bandari kubwa na ndogo, barabara kuelekea bandari hizo kutoka maeneo ya karibu na pia kuweka vituo vidogo vidogo vya biashara katika maeneo hayo.

Fedha zinazozalishwa kupitia miradi hii, zitakuwa zinazungushwa katika miradi mingine ya kijamii, kama majengo ya skuli, hospitali na vituo vya huduma za kijamii.

Hii maana yake ni kuwa, "Run Liemba" ni mradi endelevu, utawaajiri maelfu ya wakaazi wa Ziwa Tanganyika, na hivyo MV Liemba itazidi kuyagusa maisha yao ya kila siku.

Ikiwa imefanya kazi kwa miaka yote hiyo kwenye eneo hili lenye umasikini na migogoro la Ziwa Tanganyika, meli ya Liemba imekuwa ikionekana kama muokozi katika baadhi ya nyakati.

Kwa mfano, mwaka 1997 Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCCR), liliitumia meli hii pamoja na nyengine ya Muongozo, kuwasafirisha wakimbizi wapatao 75,000, ambao walikuwa wameikimbia nchi iliyokuwa ikiitwa Zaire, sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati wa vita vya kwanza vya kumuondoa Mobutu Sese Seko.

Katika operesheni hiyo iliyochukuwa wiki tano, MV Liemba peke yake ilifanya safari 22 kati ya Kigoma, Tanzania, na Uvira, Kongo.

Hili linathibitisha tu ile hoja na haja ya kuwa Liemba ni sehemu muhimu ya maisha ya watu wa eneo hili. Kwa hivyo, mradi wa "Run Liemba," lau utakuwa kama ulivyopangwa, utaakisi matakwa ndiyo, pahala ndipo na watu ndio.

Changamoto za Mradi wa "Run Liemba"

Bango la filamu ya mwaka 1951, ambayo iliihussha meli ya Liemba, African Queen
Bango la filamu ya mwaka 1951, ambayo iliihussha meli ya Liemba, African Queen

Lakini mwanasoshilojia, Franz Hiss, wa Wakfu wa Marafiki wa Liemba na mmoja wa waanzilishi wa mradi wa "Run Liemba", anasema suala lililopo mbele yao changamoto kubwa inayoukabili mradi huu kwa sasa ni mtaji wa kuufanyia kazi.

“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni namna ya kupata fedha za kuwekeza kwenye Liemba, kutoka Ujerumani na kutoka Tanzania. Vile vile, ni kwa serikali ya Tanzania kuonesha maelezo ya wazi juu ya namna fedha hizo zitakavyotumika." Anasema Franz Hiss.

Hata hivyo, kitu kimoja kinaweza kuwa cha uhakika: kiwango chochote cha fedha kitakachoingizwa ndani ya mradi huu kina nafasi kubwa ya kujilipa na kukua.

Meli ya Liemba inafanya safari zake, kwa uchache, mara mbili kwa wiki kutoka kila upande, Kigoma kwenda Mpulungu kila Ijumaa na Jumaatano na Mulungu kwenda Kigoma kila Ijumaa na Jumaapili.

Ndani yake, abiria hukaa ama kwenye daraja la kwanza au la tatu. Baina ya Kigoma na Mpulungu, husimama vituo kadhaa, ambavyo havina gati na hivyo wasafiri hulazimika kutumia mashua ndogo ndogo kuifikia ilipo.

Yote haya ni maeneo ambamo euro milioni 10 zinaweza kuwekezwa na kujikuta zikizalisha, almuradi tu pande zinazohusika zinashirikishwa na zinajitolea kwa moyo mmoja.

"Tunatarajia kwamba, mradi huu wa Run Liemba utafahamika na wenzetu wa Tanzania. Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa mradi unachangia katika maendeleo ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi ya Ziwa Tanganyika. Na tunafikiri kwamba, katika kufikisha miaka yake 100 hapo mwaka 2015, taasisi kama vile Taasisi ya Goethe, makampuni ya utalii na wawekezaji wengine wataunga mkono mradi huu." Anasema Franz Hiss.

Inakoelekea Liemba

Liemba katika Vita vya Kwanza vya Dunia
Liemba katika Vita vya Kwanza vya DuniaPicha: picture-alliance/akg-images

Wakfu wa Marafiki wa Liemba wanafanya kazi kubwa hivi sasa ya kuzifanya serikali za Ujerumani na Tanzania, pamoja na taasisi za kifedha katika nchi hizo, kama vile mabenki na mifuko ya fedha, kuona umuhimu wa kuweka fedha zake kwenye mradi wa Run Liemba.

Joseph Bwana, mmoja wa wajumbe wa Wakfu wa Marafiki wa Liemba na pia mjumbe wa bodi ya kampuni inayosimamia meli ya Liemba, anaamini kwamba kama fedha zikiingizwa kwenye mradi, mabadiliko makubwa yataonekana.

"Tunaona kuwa mradi huu ni endelevu sana, kwa hivyo kama utaendelezwa, basi utachochea mafanikio makubwa kwa watu wa eneo hili, na sisi upande wa Tanzania tumejitayarisha vyema." Anasema Bhwana.

Kwa nchi ambayo bado inajikokota kwenye umasikini, kama ilivyo Tanzania, vile tu kumudu kuifanya meli hii kuwa hai kwa kipindi chote hiki ni moja ya alama za uendelevu wa meli na mradi wenyewe.

Tangu uhuru wa Tanganyika kutoka Uingereza hapo mwaka 1961, Liemba haijawahi kusimama kufanya kazi, licha ya kuwepo kwa miradi mingi mipya zaidi nchini humo, ambayo ilianzishwa na kufa ndani ya kipindi kifupi.

Lakini roho ya Liemba imethubutu kupasi majaribu ya nyakati. Ndivyo pia unavyotarajiwa mradi wa "Run Liemba" kama wajumbe wa Wakfu wa Marafiki wa Liemba wanavyotaraji, kwamba meli ya Liemba kamwe haitakufa.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo