1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa barani Ulaya yazidi kunguruma

Sekione Kitojo21 Oktoba 2010

Inter Milan ilifanikiwa kuzima moto wa Tottenham Hotspurs ya Uingereza kutaka kurejea nyumbani angalau na points moja.

https://p.dw.com/p/PjbM
Wesley Sneijder, wa Inter Milan akishangilia bao pamoja na wenzake Maicon, na Samuel Eto'o.Picha: AP

Samuel Eto'o alifumania nyavu mara mbili katika ushindi wa mabao 4-3 kwa mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa barani Ulaya Inter Milan baada ya kuhimili vishindo vya Tottenham Hotspur ya Uingereza jana usiku, wakati Nani aliondoa ukungu uliotanda katika klabu ya Manchester kuhusu kipenzi cha klabu hiyo Rooney kukiwa na uvumi kuwa anataka kuihama klabu hiyo.

Pambano ambalo halikuwa la kawaida katika uwanja wa San Siro lilikuwa ni pambano la duru ya tatu ya michuano ya kundi A hadi D wakati Tottenham waliporuhusu magoli matatu katika muda wa dakika 15, na mlinda mlango wa timu hiyo alitolewa nje kwa kadi nyekundu , lakini hata hivyo nusura warejee nyumbani Uingereza na point moja baada ya Gareth Bale kupachika mabao 3 .

Nani aliweka wavuni bao maridadi la ushindi katika ushindi wa bao 1-0 wa Manchester United dhidi ya Bursaspor ya Uturuki katika kundi C katika uwanja wa Old Traford huku magoli mawili ya Lionel Messi yakiipa Barcelona ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Copenhagen katika uwanja wa Nou Camp na kuchukua uongozi wa kundi D.

Katika kundi B Raul , ambaye ni mchezaji anayeshikilia rekodi ya kupachika mabao mengi zaidi katika ligi ya mabingwa , alifikisha jana mabao 68 kwa kupachika bao katika kila kipindi kwa timu yake ya Schalke 04 ya Ujerumani wakati Hapoel Tel Aviv ya Israel ikisalim amri kwa mabao 3-1.

Champions League 20.10.2010 FC Schalke 04 - Hapoel Tel Aviv
Mshambuliaji Raul wa Schalke 04 akishangilia bao dhidi ya Hapoel.Picha: AP

Kuweza kufunga mabao mawili katika mchezo muhimu kama huo , yakiwa magoli ya kwanza tangu kujiunga na Schalke katika champions League kunanifanya nijisikie vizuri, amesema Raul. Sikuweza kufikiri iwapo nitafikisha kiwango cha magoli 68. Hii ni siku ambayo nitaikumbuka sana, Mhispania huyo amewaambia waandishi habari.

Schalke inafuatia nyuma ya Olympique Lyon ambao wamefikisha points tisa kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Benfica ya Ureno. Klabu hiyo ya Ufaransa ni moja kati ya timu tano zikiwa zimefanikiwa kushinda michezo yao yote mitatu katika kinyang'anyiro hicho.

Rangers wameweka matumaini yao hai ya kupata nafasi ya kushiriki katika timu 16 zitakazoingia katika duru ya mtoano kwa sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Valencia na kushika nafasi ya pili nyuma ya Manchester United katika kundi la C.

Panathinaikos Athen ilitoka sare ya bila kufungana na Rubin Kazan katika kundi D, matokeo ambayo hayakusaidia nafasi kwa pande zote mbili kuweza kuonyeshana misuli na Barcelona na Copenhagen katika nafasi za juu.

Twente Enschede ilitoka sare nayo ya bao 1-1 dhidi ya Werder Bremen lakini huu ulikuwa mchezo wa kundi A.

Kumaliza kwa Tottenham msimu uliopita katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ya Uingereza , Premier League kulichangia kushusha pazia la enzi za kutamba kwa kocha Rafael Benitez katika kilabu ya Liverpool. Kocha huyo raia wa Hispania amekalia kiti moto katika klabu ya Inter Milan akitakiwa kufuata nyayo za Jose Mourinho, na jana alionekana kuelekea kumpa kibano cha nguvu kocha wa Tottenham Harry Redknapp katika dakika 35 za kwanza wakati Inter ilipokuwa tayari ina mabao 4.

Ilikuwa ni kama umeshikwa na jinamizi baya, amesema Redknapp, wakati timu yake ilikuwa nyuma kwa mabao 4-0 katika nusu ya kwanza ya mchezo.

Wakati huo huo meneja wa Manchester United Alex Ferguson atakutana na mwenyekiti mtendaji David Gill leo Alhamis wakati akijaribu kuzuwia mipango ya Wayne Rooney kutaka kuihama klabu hiyo kuwa msururu wa matukio ya vituko.

Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE