1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya Mabingwa Ulaya:Bremen yaepuka kipigo nyumbani,Inter,MANU ngoma nzito

Aboubakary Jumaa Liongo15 Septemba 2010

Werder Bremen jana ilionesha ushupavu mkubwa pale iliposawazisha mabao 2 iliyokuwa imefungwa na Totenham Hotspur katika pambano lililokuwa kali na kusisimua.

https://p.dw.com/p/PCTK
Marko Marin wa Bremen akishangilia bao la pili.Picha: AP

Bremen ikicheza nyumbani ilishuhudia Tottenham ikipata mabao mawili ya harakaharaka mwanzoni mwa mchezo katika dakika ya 12 na 18 kupitia kwa Peter Crouch huku Petri Pasanen akijifunga mwenyewe.

Dakika mbili kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, Hugo Almeida alifufua matumaini kwa kuipatia Bremen bao la kwanza kwa kichwa, ambapo katika kipindi cha pili, Bremen ilicharuka na kusawazisha bao hilo kupitia kwa  Marko Marin.Marin mchezaji mfupi mwenye kasi na chenga alionekana kuwa mwiba kwa Tottenhamn.

Fußball Champions League Schalke Lyon
Mbrazil Michel Bastos wa Lyon kushoto na Christoph Moritz wa Schalke kulia wakiwania mpira .Picha: AP

Wawakilishi wengine wa Ujerumani katika michuano hiyo Schalke 04 walichapwa bao 1-0 na Olympique Lyon ya Ufaransa mjini Paris.Schalke ililazimika kucheza pungufu muda mwingi wa mchezo baada ya mchezaji wake Benedikt Hoewedes kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 38.

Nao mabingwa watetezi  Inter Milan walianza safari yao ya kutetea ubingwa huo kwa kulazimishwa sare na Twente Enschende ya mabao 2-2.

Manchester United ikicheza nyumbani ilikumbana na ukuta mgumu wa Rangers na kulazimishwa suluhu bin suluhu.Kocha wa United Sir Alex Furgeson alipanga kikosi dhaifu, akiwaweka nje  Dimitar Berbatov  pamoja mkongwe katika kiungo Paul Scholes.

Lakini Barcelona ilifanya mauaji makubwa baada ya kuichabanga Panathinaikos mabao 5-1 mjini Barcelona, huku  jogoo wao Lionel Messi akipachika mabao mawili pamoja na kukosa penalti.

Katika mechi nyingine hiyo jana Valencia ikiwa ugenini ilifuata nyanyo za wenzao Bareclona kwa kuwachapa Bursaspor mabao 4-0.Nayo  Benfica ikiwa nyumbani iliifunga Hapoel Tel Aviv mabao 2-0, huku  FC Copenhagen ikiutumia vizuri uwanjani wake wa nyumbani kwa kuifunga Rubin Kazan bao 1-0.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA

Mhariri:Mohamed Abdulrahman