1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lini vita ya Sudan vitapatiwa suluhu?

18 Machi 2012

Vita vilivyojificha vinavyoathiri maelfu ya watu wakati hofu ikizidi kupanda baina ya Sudan na Sudan Kusini, vinatishia kuwa machafuko makubwa, kwa mujibu wa maelezo ya wachambuzi na wanadiplomasia.

https://p.dw.com/p/14MMt
Msanii wa filamu George Clooney alikamatwa hivi karibuni katika ubalozi wa Sudan Marekani, akipinga ghasia za Sudan.
Msanii wa filamu George Clooney alikamatwa hivi karibuni katika ubalozi wa Sudan Marekani, akipinga ghasia za Sudan.Picha: Reuters

Mapigano kati ya waasi wa kabila la Nuba na vikosi vya serikali katika jimbo la Kordofan Kusini mwezi Juni, mwaka jana, mwezi mmoja kabla ya uhuru rasmi wa Sudan Kusini yameleta athari kubwa kwa wa eneo hilo.

Wanuba walikuwa washirika wa waasi wa Kusini wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 22, ambavyo viliishia mwaka 2005 kabla ya kura ya maamuzi ya mwezi Januari 2011.

Lakini Khartoum ilitoa tuhuma kwamba serikali mpya ya Kusini inaendelea kuwasaidia waasi wa Chama cha Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N) jimboni Kordofan Kusini.

Khartoum ilitishia kulipiza kisasi juma lililopita baada ya kuishutumu Kusini kwa kuunga mkono shambulio la waasi katika eneo la mpaka lenye machafuko, Jau.

Mwanahabari Lubna Hussein, wa asili ya Kifaransa na Kisudan, yuko mstari wa mbele kupinga ukiukwaji wa haki nchini Sudan.
Mwanahabari Lubna Hussein, wa asili ya Kifaransa na Kisudan, yuko mstari wa mbele kupinga ukiukwaji wa haki nchini Sudan.Picha: AP

Mwanadiplomasia mmoja kutoka mataifa ya Magharibi ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema machafuko yanayoendelea Sudan zote mbili yanaweza kuathiri eneo zima na kuwa vita kamili.

Khartoum imesema waasi waliosindikizwa na maofisa wa kutoka Jeshi la Sudan Kusini walifanya shambulizi la moja kwa moja, lakini Juba imepinga kuyasaidia makundi ya upinzani nchini Sudan na ikaongeza kuwa Jau ni sehemu ya mpaka wake.

Mwanzoni mwa mwezi Machi, mwaka huu, Kusini ilitoa tuhuma kuwa ndege za kivita za MiG zilivishambulia visima vya mafuta na maji, kilomita 74 ndani ya mpaka wake wakati vikosi vya ardhini vilipospgea umbali wa kilomita 17, ndani ya Jimbo la Unity, lenye utajiri wa mafuta.

Khartoum imekana madai hayo, lakini Marekani imetoa onyo. Imesema matukio hayo hayakubaliki na yanatishia kuzusha ghasia zaidi baina ya pande hizo mbili.

Magdi El Gizouli wa Taasisi ya Rift Valley, amesema shambulio la kwanza la Jau lisingetokea kama Jeshi la Sudan Kusini lisingeanzisha chokochoko.

Gizouli anaona mapigano hayo ni mwendelezo wa chuki iliyopo baina ya mataifa hayo mawili yanayogombana juu yaa ada za mafuta na masuala mengine, yaliyoibuka kufuatia Kusini kujitenga.

Sudan Kusini ilipopata uhuru wake, ilimiliki robo tatu ya uzalishaji wa mafuta ya Sudan lakini haina miundombinu yake binafsi ya kuzalisha nishati hiyo. Nchi hizo zimeshindwa kukubaliana kiasi cha fedha ambazo Juba inapaswa kulipa kwa ajili ya kutumia bandari na bomba la kusafirishia mafuta hayo.

Ni baadhi ya wakazi wa Kambi ya Abu Shouk, Kaskazini mwa Darfur, inayowatunza zaidi ya raia 40,000 waliokosa makazi.
Ni baadhi ya wakazi wa Kambi ya Abu Shouk, Kaskazini mwa Darfur, inayowatunza zaidi ya raia 40,000 waliokosa makazi.Picha: AP

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amemshtumu Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, kuwa anajaribu kuikandamiza Sudan Kusini.

Mwanadiplomasia mmoja ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa kuwa Juba "inacheza mchezo hatari" kwa kuyaunga mkono makundi ya waasi na kutaka kuuangusha utawala wa Khartoum.

Mshauri wa makanisa ya Sudan kwa muda wa miaka 29 sasa, John Ashworth, amesema serikali ya Sudan imewazuia kabisa wanahabari, wanadiplomasia na mashirika ya misaada kuingia katika uwanja wa vita, lakini Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya raia 360,000 hawana makazi au wameathirika sana na ghasia hizo katika jimbo la Kordofan Kusini na jirani na jimbo la Blue Nile.

Si Umoja wa Mataifa wala Shirika la Msalaba Mwekundu inayoweza kusema ni watu wangapi ambao si wapiganaji, wamepoteza maisha tangu mwezi Juni, mwaka jana, katika machafuko hayo, yanayodaiwa kufanywa na jeshi la Sudan Kaskazini kutokea angani, japo Khartoum inapinga.

Mwandishi: Pendo Paul\ AFP

Mhariri: Sekione Kitojo