1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liu Xiang aipatia China dhabu

Ramadhan Ali31 Agosti 2007

Liu Xiang amenyakua leo medali ya dhahabu katika mita 110 kuruka viunzi huku Jeremy Wariner akiikosea kidogo kuifuta rekodi ya dunia ya mita 400 ya Michael Johnson.

https://p.dw.com/p/CHb5
Liu Xiang bingwa mita 110 viunzi
Liu Xiang bingwa mita 110 viunziPicha: AP

Mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia mjini Osaka,Japan, yakifikia kilele chake mwishoni mwa wiki hii,Jeremy Wariner wa Marekani na Liu Xiang wa China wametawazwa alaasiri ya leo mabingwa wa dunia kama ilivyotazamiwa.

Mkenya Alfred Kirwa Yego ameongoza mbio za mita 800 kabla finali ya jumapili huku bingwa wa dunia mzaliwa wa Morocco anaekimbia chini ya bendera ya Bahrein,Rashid Ramzy, amepigwa kumbo nje ya finali zote 2-mita 800 na 1500.

Ramadhan ali anawachukua Osaka kusikia mapya jioni hii:

Muamerika Jeremy Wariner, aliikosea kidogo tu kuifuta hii leo rekodi ya dunia ya mita 400 ya Michael Johnson ya sek.43.18 alipotoroka leo na medali ya dhahabu katika masafa hayo.

Muda wake yeye ulikuwa sek.43.45-muda bora msimu huu.Mwenzake LaShawn Merrit, alikuja wapili huku muamerika mwengine Angelo Taylor, akichukua medali ya shaba.

China, itakayoandaa michezo ijayo ya olimpik mjini Beijing 2008, ilitwaa nayo medali yake ya kwanza ya dhahabu alaasiri ya leo pale bingwa wao wa Olimpik katika mita 110 kuruka viunzi Liu Xiang, alipozima vishindo vya Terrence Trammell wa Marekani huku David Payne akibidi kuridhika na medali ya shaba.Muda wa Liu Xiang ulikua sek.12.95.

Katika changamoto ya mita 200 wanawake, msichana wa Marekani, Allyson Felix alitimka mbio na kumaliza mbio hizo chini ya sek. 22 ikiwa ni mara ya kwanza tangu Inger Miller pia wa Marekani kufanya hivyo 1999.

Medali ya pili ya dhahabu kwa bingwa wa mita 100 kutoka Jamaica Veronica Campbell, haikuwapo leo,kwani Felix hakuitoa.Muda wake wa ushindi leo ulikua sek.21.81.

Campbell alibidi kuridhika na medali ya fedha mara hii huku ile ya shaba ikienda kwa msichana wa Sri Lanka, Susanthika Jaysinghe.

Cuba iliifuata Panama jana,kwa kunyakua leo medali ya dhahabu katika kuchupa mara tatu-Tripple jump.Masafa yake yalikua mita 15.28.Yargelis Savinge wa Cuba alimzima hapo Tatyana Lebedeva wa Russia kutwaa kwa mara ya pili taji hilo.

Medali ya dhahabu katika kurusha mkuki imekwenda kwa Barbora Spotaklova wa Jamhuri ya Czech.

Kesho itakua finali ya mita 5000 wanawake ambamo bingwa wa olimpik Meseret Defar wa Ethiopia, anatumai kuwika.Mkenya Alfred Kirwa Yego, anatazamia pia kuipatia Kenya medali ya dhahabu katika mita 800 hapo jumapili baada ya bingwa wa mbio hizi Rashid Ramzy wa Bahrein, kuvuliwa taji na mapema.Ramzy,alishindwa katika nusu-finali na amepoteza mataji yote 2 ya dunia-mita 800 na 1.500.