1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Livni ameshindwa kuunda serikali ya muungano

Kalyango Siraj20 Oktoba 2008

Rais amemuongezea mda zaidi wa siku 14

https://p.dw.com/p/Fden
Tzipi Livni, kushoto na Ehud Olmert, kuliaPicha: AP

Rais wa Israel amempa muda zaidi wa wiki mbili, waziri wa mashauri ya kigeni wa nchi hiyo Tzipi Livni wa kuweza kuunda serikali kuchukua pahala pa ile iliokuwa inaongozwa na Ehud Olmert aliejiuzulu.

Livni ndie kiongoni mpya wa chama tawala cha Kadima na hivyo alipashwa kuunda serikali hadi jumatatu. Lakini tangu Septemba 22 wakati Bw Olmert alipojiuzulu kutokana na madai ya rushwa hadi kufikia jumatatu asubuhi alikuwa hajaunda serikali ya muungano na mda aliokuwa amepewa na rais wa kuunda serikali hiyo ulikuwa unaisha.Kulikuwa na hofu kuwa kushindwa kwake kungesababisha kuitishwa kwa uchaguzi mkuu wa mapema.

Akiwa katika mchakamchaka wa kuunda serikali, Bi Livni anasemekana ameomba kupewa muda zaidi. Na ombi lake limekubaliwa na rais wa Israel Shimon Perez.

Taarifa iliotolewa na ofisi ya Bw Perez imesema kuwa Bi Livni amekutana kwa mazungumzo na rais kwa mda wa saa moja na dakika 15, jumatatu asubuhi na kumuelezea kuhusu juhudi zake za kuunda serikali ilioitwa imara na ya muda mrefu katika muda wa siku 28 alizopewa mwanzo.Chini ya sheria za Israel, mbali na kupewa muda wa siku 28 lakini pia anaweza kuomba kuongozewa muda zaidi wa siku 14 ambao aliutumia jumatatu asubuhi.

Ingawa Livni alisema alipanga kuunda serikali mpya ya mseto haraka iwezekanavyo lakini hakufanikiwa kukubaliana na makundi yanayotosha kumuwezesha kuunda serikali hiyo.Miongoni mwa makundi hayo yanayoonekana kumgomea ni chama cha Shas. Hali halisi inaelezwa na kauli ya mbunge wa chama cha Kadima Tzachi Hanegbi,ambae amesema kuwa hawatakubali kutiwa kishindo.

Chama cha Shas, ambacho kinadai kuwakilisha maslahi ya walala hoi,kimekuwa kinaomba serikali iongeze dau, katika matumizi yake ya dola millioni 270,kwa huduma za jamii,ili kuweza kujiunga na serikali inayoongozwa na Bi Livni

Swali muhimu hapa ni ikiwa Livni, ambae tayari amepata uhakikisho wa awali na chama cha waziri wa Ulinzi Ehud Barak cha Leba, kushirikiana katika serikali ya muungano anaweza mara hii akakishawishi cha msimamo mkali cha Shas kuweza kumkubalia kuungana nae.

Bi Livni ikiwa ataungwa mkono na vyama vidogovidogo kama vile chama cha waliostaafu,kilicho na wabunge saba pamoja na kile cha mrengo wa kushoto cha Maretz ambacho kinawabunge watano,kutampa nguvu za kuendeleza sera zake mkiwemo kujadilia amani na wa palestina.

Na inatarajiwa kuwa majadiliano kati ya chama cha Kadima na Shas yakaanza upya,huku kukiwa na fununu kuwa Livni anapanga kuunda serikali wakati bunge litakapo itisha kikao Okt 27 baada ya likizo ya majira ya kiangazi.

Bila uungaji mkono wa chama cha Shas Livni ataunda serikali ya wachache na kutegemea msaada wa tahadhari kutoka nje ya muungano kutoka kwa wafuasi wa mrengo wa kushoto na pia vyama vya waarabu,la sivyo kura za maoni zinaonyesha kuwa chama cha mrengo wa kulia cha Likud cha Benjamin Netanyahu kinaweza kushinda uchaguzi.

Na ikiwa Livni atashindwa kuunda serikali, bila shaka kutaitishwa uchaguzi wa mapema kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa mwaka wa 2010.