1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

London. Bhutto kurejea Pakistan.

2 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBTY

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto amesema kuwa atarejea nchini mwake kutoka uhamishoni alikoishi kwa muda wa miaka kadha , licha ya kushindwa kufikia makubaliano ya kugawana madaraka na rais Pervez Musharraf.

Bhutto amewaambia waandishi wa habari mjini London kuwa atatangaza tarehe ya kurejea kwake hapo Septemba 14.

Bibi Bhutto amesema kuwa amekuwa na mtazamo tofauti na rais Musharraf kuhusu uhuru wa taasisi ya bunge pamoja na uchaguzi unaohusu kiti cha urais pamoja na waziri mkuu. Lakini ameongeza kuwa hayo ni masuala ambayo alikuwa anaamini yanaweza bado kuendelea kujadiliwa. Lakini baada ya hapo mambo yalianza kukwama.

Generali Musharraf alituma wasaidizi wake mjini London mapema jana katika juhudi za kuyanusuru makubaliano hayo. Bhutto ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ulaji rushwa, amewalaumu watu wenye msimamo mkali katika chama cha rais Musharraf kwa kuchafua mazungumzo hayo.

Waziri mwingine mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Shariff, pia anapanga kurejea nchini humo kugombea katika uchaguzi mkuu ujao.