1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Blair anaendelea kupigia debe mkakati mpya

15 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCsg

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair ameiambia Marekani,njia ya kuzishirikisha nchi za kiislamu zenye siasa za wastani katika mpango wo wote ule mpya kuhusu Irak,ni kusuluhisha mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina.Amesema,suluhisho lolote kuhusu Irak lazima liwe sehemu ya mkakati wa Mashariki ya Kati nzima.Blair alitamka hayo alipozungumza kwa mawasiliano ya video na jopo la Kimarekani lililoundwa kuichunguza upya sera ya Marekani nchini Irak.Jopo hilo lenye wajumbe wa Republikan na Demokrat,mwezi ujao linatarajiwa kuwasilisha katika Ikulu ya Marekani ripoti yake ya ushauri kuhusu Irak.Msemaji wa serikali ya Uingereza mjini London amesema Blair amesisitiza kuwa mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina ni kipaumbele katika Mashariki ya Kati.Matamshi ya Blair yalirudia hotuba yake muhimu ya siku ya Jumatatu.Katika hotuba hiyo Blair alitoa mwito wa kufanywa mabadiliko katika mkakati wa Mashariki ya Kati na alizihimiza Syria na Iran zishiriki katika mkakati huo mpya.