1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

London. Brown achaguliwa kuiongoza Labour.

25 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBob

Gordon Brown amethibitishwa katika kura ambayo hakuwa na mpinzani akiwa kiongozi mpya wa chama tawala cha Labour nchini Uingereza siku chache kabla ya kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

Katika mkutano maalum mjini Manchester , Brown amewaambia wajumbe wa chama cha Labour kuwa chama hicho kinahitaji mabadiliko.

Amesema kuwa atajifunza kutokana na uamuzi wa Tony Blair kuingia vitani nchini Iraq lakini ametoa ishara chache kuwa sera zake kuelekea ugaidi zitatofautiana kwa kiasi kikubwa na zile za mtangulizi wake.

Amesema kuwa kuwapo kwa Tony Blair katika medani ya kimataifa, kumemfanya kufanyakazi kwa ajili ya Afrika, mabadiliko ya hali ya hewa na pia amefanyakazi kuiletea Uingereza michezo ya Olympic. Na tusisahau amesisitiza mbinu na msukumo aliokuwa nao pamoja na uvumilivu hadi kuleta amani katika Ireland ya kaskazini.

Katika masuala ya ndani , amesema kuwa afya, elimu na kufutwa kwa umasikini wa watoto yatakuwa masuala atakayoyapa umbele.

Uchaguzi wa Brown kuwa kiongozi wa chama cha Labour unakipa chama hicho msukumo katika maoni ya umma baada ya kuathirika kutokana na vita vya Iraq ambavyo vimewakera wapiga kura.