1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Brown asema wakati wa uchaguzi bado

3 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBSu

Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amesema leo kwamba wakati haujafika kwa Uingereza kufanya uchaguzi mkuu, lakini akakataa kufutilia mbali uwezekano wa kuitisha uchaguzi kabla mwaka huu kumalizika.

Huku kura ya maoni ikionyesha umaarufu wake ukishuka ikilinganishwa na wakati alipochukua madaraka mwezi Juni kutoka kwa waziri mkuu wa zamani, Tony Blair, Gordon Brown amesema hatatizwi na wakati wa kuitisha uchaguzi mkuu, bali anafanya bidii kutimiza wajibu wake.

Hapo awali Gordon Brown alisema kuondoka kwa kikosi cha mwisho cha Uingereza kusini mwa Irak hakuashirii kushindwa, akiongeza kuwa hatua hiyo ilipangwa kabla kuchukuliwa.

Msemaji wa kikosi cha Uingereza mkoani Basra, Mark Shearer, amesema kuondoka kwao ni hatua itakayosaidia kuwapa wanajeshi wa Irak jukumu la kuulinda mkoa wote wa Basra baadaye mwaka huu, lakini akasema kwa sasa bado wana jukumu la kuhakikisha usalama.

´Nadhani jambo la muhimu kutambua ni kwamba bado tuna dhamana kuhusu usalama wa mkoa wa Basra na hivyo mji wa Basra. Hiyo ina maana tutachagua mikakati ya operesheni zetu mjini humo tukizingatia kwamba vikosi vya Irak viko tayari kuulinda mji huo vyenyewe.´

Na habari za hivi punde nchini Irak zinasema mwanajeshi mmoja wa Marekani ameuwawa wakati bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara kulipuka karibu na msafara wao wa magari karibu na mji mkuu Baghdad.