1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

London. Brown haondoi uwezekano wa kujiunga na juhudi za kimataifa dhidi ya Iran.

8 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7HU

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesema leo kuwa haondoi uwezekano wowote katika juhudi za kimataifa kuifanya Iran kujitenga na utengenezaji wa silaha za kinuklia.

Brown amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa nia ya Iran ya kuwa na teknolojia ya kinuklia haitakwenda bila ya kupingwa.

Alipoulizwa iwapo hatajiunga na uwezekano wa hatua za kijeshi zinazoanishwa na Marekani dhidi ya Iran, Brown amesema , anachoweza kusema ni kwamba wanachukulia kwa dhati kile ambacho Iran inapendekeza, na haondoi uwezekano wa kitu chochote.

Matamshi yake yamekuja wakati kuna ripoti kuwa Iran na umoja wa Ulaya wanatarajia hivi karibuni kuanza tena mazungumzo kuhusiana na suala hilo la kinuklia. Kuhusu kuitisha uchaguzi na mapema nchini Uingereza kutokana na kupanda umaarufu wake, waziri mkuu Gordon Brown amesema , kwanza anataka kupanga mikakati ya kuiongoza nchi katika ufanisi.