1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Mataifa makuu kufuatilia vikwazo dhidi ya Iran

7 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD5P

Mataifa sita makubwa duniani yamekubaliana hapo jana kufuatilia suala la kuwekewa vikwazo Iran kutokana na mpango wake wa nuklea lakini imetowa tu taarifa isio kali ambayo imewacha bila ya ufumbuzi masuala ya ukubwa na wakati wa kuchukuliwa kwa hatua hizo za vikwazo.

Wanadiplomasia waandamizi kutoka Marekani,Uingereza, Ufaransa,Ujerumani,China na Russia wamesema katika taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo hayo mjini London kwamba wamevunjwa moyo sana na kugoma kwa Iran kusitisha urutubishaji wa uranium ambayo ni hatua muhimu katika kutengeneza silaha za nuklea.

Zikionekana kugawika juu ya namna ya kuchukuwa hatua ya haraka wanadiplomasia hao wamesita kutangaza wazi kwamba mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na Iran yameshindwa kufanikiwa.

Taarifa yao hiyo pia imeipuka kudai kwamba Iran iadhibiwe na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakini imesema watajadili suala la vikwazo katika mazungumzo kwenye Umoja wa Mataifa.

Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Alexander Alexeyev amesema suala la kutumia nguvu dhidi ya Iran halitokubaliwa.