1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Polisi yateguwa bomu kwenye gari

29 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBnJ

Polisi ya Uingereza imesema kwamba imezima mripuko wa bomu katikati ya London leo hii.

Polisi imesema katika taarifa kwamba wataalamu wa mabomu waliitwa kuchunguza gari aina ya Merecedes lililoegeshwa kwenye Haymarket mtaa wenye harakati kubwa katikati ya eneo lenye majengo mengi ya kumbi za sinema na michezo ya kuigiza mapema leo asubuhi.

Taarifa hiyo imesema wamegunduwa kile kinachoonekana kama kifaa kinachoweza kuripuka ambacho waliweza kukidhibiti na kwamba maafisa wa kupambana na ugaidi wanaendelea na uchunguzi kwenye mtaa huo ambao umefungwa na yumkini ukaendelea kufungwa kwa muda mkubwa ujao.

Msemaji wa polisi amethibitisha kwamba hilo lilikuwa ni bomu.

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesema kugunduliwa kwa bomu hilo kunaonyesha jinsi Uingereza inavyoendelea kukabiliwa na tishio zito kutoka ugaidi.

Amesema wananchi wanatakiwa kuwa macho na hali hiyo ya kuwa macho inafaa kuendelezwa kwa siku kadhaa zijazo.

Brown amesema waziri mpya wa Mambo ya Ndani Jacqui Smith atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa kamati ya dharura ya serikali inayojulikana kama Cobra na kurepoti kwa baraza la mawaziri baadae leo hii.