1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Sakata la kifo cha Litvinenko lapamba moto

1 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCns

Polisi ya Uingereza na majasusi wa nchi hiyo wanatuhumu kwamba wahuni fulani ndani ya jamii ya Urusi wanahusika na kifo cha mpelelezi wa zamani wa Urusi Alexander Litvinenko kutokana na sumu.

Gazeti la Guardian limeripoti leo hii kwa kukariri duru isizozitaja majina ndani ya polisi na majasusi zikisema kwamba wapelelezi wanawafuatilia kundi la wanaume watano au zaidi waliowasili mjini London kutoka Moscow muda mfupi kabla ya Litvinenko kuanza kuuguwa.Litvinenko alifariki wiki iliopita.

Ndege nne zinafanyiwa uchunguzi wa kuwepo kwa sumu ya miale ya nuklea.Shirika la ndege la Uingereza linasema linataka kuwasiliana na abiria 33,000 na wafanyakazi 3,000.Ndege tatu zilizoondolewa kwenye safari zilikuwa zimeruka kati ya Moscow na London na ndege ya nne ilikuwa imekodishwa na shirika la ndege la Urusi la Transaero.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza John Reid ameliambia bunge alama za sumu za miale ya nuklea zimeonekana kwenye sehemu 12 kati ya 24 alizotembelea Litvinenko.

Wakati huo huo waziri mkuu wa zamani wa Urusi na mwanamageuzi wa masoko Yegor Gaidar inasemekana kuuguwa kwake kumetokana na sumu.Gaidar alizirai akiwa nchini Ireland na hivi sasa yuko hospitalini mjini Moscow.