1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON:Polisi wa metropolitan wapatikana na hatia

2 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C7AZ

Polisi wa Metropolitan wa London nchini Uingereza wamepatikana na hatia ya kukiuka sheria za usalama baada ya kumpiga risasi hadi kufa raia mmoja wa Brazil kwa kumdhania kuwa mlipuaji wa kujitoa muhanga.Jean Charles de Menezes alipigwa risasi mwaka 2005 katika kituo cha treni cha Stockwell kusini mwa mji wa London.Jaji Richard Henriques alipiga faini polisi wa London euro laki mbili hamsini na mbili aidha kuwaagiza kulipa gharama za paundi alki tatu themanini na tano.

Uamuzi huo wa mahakama umezua hisia tofauti na wito wa kujiuzulu kwa mkuu wa Polisi wa London Sir Ian Blair.Bwana Blair anashikilia kuwa hatajiuzulu na kuongeza kuwa maafisa waliokuwa kazini wakati huo walichukua hatua iliyokuwa bora katika mazingira waliyokuwamo.

Wizara ya mambo ya nje ya Brazil imepongeza uamuzi huo kwani unaonyesha uwajibikaji wa polisi wa Uingereza aidha unafungua njia ya kuwezesha familia ya de Menezes kutendewa haki

Jean Charles de Menezes aliyekuwa na umri wa miaka 27 alipigwa risasi saba kichwani tarehe 22 mwezi Julai mwaka 2005 katika kituo kimoja cha treni za chini kwa chini mjini London.Mfumo wa treni za chini kwa chini mjini London ulikuwa umekabiliwa na shambulio majuma mawili kabla ya tukio hilo.Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu 52.Polisi walimfananisha de Menezes na Hussain Osman aliyedaiwa kuhusika na njama ya mashambulizi hayo.Bwana Osman alitumikia kifungo cha maisha kilichoanza mwanzoni mwa mwaka huu.