1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON:Virusi vya maradhi ya miguu na midomo huenda vimesambazwa na binaadamu

8 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBb3

Virusi vilivyosababisha mlipuko wa maradhi ya midomo na miguu katika mashamba mawili ya mifugo huko kusini mwa Uingereza huenda vilitoka katika maabara iliyojirani na maeneo hayo.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti kamati ya usalama wa afya ya Uingereza.

Imesema kuwa huenda vilisambazwa na binaadamu, na kusema kuwa uwezekano wa hewa kuchangia kusambaza virusi hivyo ni mdogo.

Virusi hivyo vilibainika kwa mara ya kwanza Ijumaa wiki iliyopita, kabla ya taarifa ya kubainika katika shamba la pili la mifugo juzi jumatatu.

Mashamba yote mawili ya mfugo yako kilomita chache kutoka katika maabara ya serikali pamoja na ile inayoendeshwa na kampuni binafsi ya madawa.

Wakati huo huo China imepiga marufuku uingizwaji wa bidhaa za mifugo pamoja na mifugo yenyewe kutoka Uingereza.

Idara ya serikali ya nchi hiyo inayohusika na usalama wa vyakula imesema kuwa marufuku hiyo inatokana na Uingereza kukumbwa na maradhi hayo ya miguu na midomo kwa mifugo.

Katika hatua nyingine watalaam wa mifugo kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kuangalia uwezekano wa kulegeza marufuku ya uingizwaji wa nyama na mifugo katika nchi hizo kutoka Uingereza.

Umoja huo wa Ulaya hapo siku ya Jumatatu ulitangaza kupinga marufuku bidhaa za mifugo na mifugo yenyewe kutoka Uingereza.