1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lufthansa:Marubani wagoma Ujerumani

22 Februari 2010

Usafiri wa ndege umetatizika hapa Ujerumani baada ya marubani alfu 4 wa shirika la ndege la Lufthansa kuanza mgomo wa siku nne.Safari za ndege za kuelekea kote hapa barani Ulaya pamoja na Marekani zimevunjwa.

https://p.dw.com/p/M7jD
Marubani ndegeni:Tumesusa!


Mgomo huo umeandaliwa na chama cha marubani,Cockpit.Hata hivyo safari za kuelekea Afrika,Amerika ya Kusini na Asia bado zinatarajiwa kuwako.Huu ni mgomo mkubwa zaidi kuwahi kufanyika katika historia ya kampuni hio.Mgomo huo utakaodumu kwa siku nne umezikwamisha shughuli za usafiri kote barani Ulaya.Kiasi cha safari 800 huenda zikavunjwa kila siku hadi mgomo utakapokamilika.Marubani hao waliamua kuchukua hatua hii baada ya mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kati ya chama chao na uongozi kuambulia patupu.Kulingana na shirika la Lufthansa huu ni mgomo mkubwa zaidi kufanyika katika historia ya Ujerumani. Msemaji wa shirika la ndege la Lufthansa,Klaus Walther alithibitisha kuwa,''Hatujawahi kushuhudia hali kama hii katika historia ya usafiri wa ndege hapa Ujerumani.Tunasikitishwa na athari wanazozipata wasafiri,shirika na hali nzima ya biashara kwa kweli.''

Vorstandsvorsitzender Wolfgang Mayrhuber Lufthansa
Mkurugenzi mkuu wa Lufthansa Wolfgang MayrhuberPicha: picture-alliance/ dpa

Mgomo wanukia Uingereza

Kwa sasa wasafiri wamepangiwa safari nyengine mpya katika mashirika mengine ya ndege au hata treni za hapa Ujerumani.Wakati huohuo hatma ya wahudumu wa shirika la ndege la Uingereza British Airways inasubiriwa hii leo.Endapo muafaka hautofikiwa wahudumu hao nao pia wanajiandaa kugoma.Chanzo cha mgomo huu wa marubani wa Lufthansa ni wasiwasi kwamba shirika hilo huenda likawapunguzia ajira kwa kuwaajiri wafanyakazi katika mataifa mengine kama Shirika la Ndege la Austria na tawi lake la Italia ili kubana matumizi.Kama anavyoeleza Alexander Gerhard-Madjiji kiongozi wa chama cha marubani,Cockpit,''Tunadai nyongeza ya mshahara na wametuahidi kiasi tu maalum pia tuyafutilie mbali madai mengine.Kulingana na mikataba tuliyonayo kwa sasa bado hatujafikia asilimia 12 ya tunachotaka kulipwa.Kwa sasa mikataba yetu inaigharimu  kampuni chini ya asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka uliopita.Hakuna fani nyengine ambayo inalipwa kiasi kama hiki chetu'' ,alisisitiza.

Deutschland Verkehr Lufthansa Streik Flash-Galerie
Ndege ya LufthansaPicha: DW/Nelioubin

Chama cha wafanyakazi kiliunyoshea mkono uongozi kwa kutaka kufanya mazungumzo mapya jambo ambalo halikuridhiwa na upande wa pili.Kulingana na uongozi wa Lufthansa mazungumzo hayatofanyika mpaka marubani hao wayafutilie mbali madai yao ambayo inaaminika yanaingilia maamuzi ya uongozi wa kampuni. Kwa sasa wasafiri wamepangiwa safari nyengine mpya katika mashirika mengine ya ndege au hata treni za hapa Ujerumani.

Fedha taslimu

Pande zote mbili zinaendelea na misimamo yao ya kutaka masharti yatimizwe ndipo mazungumzo mapya yafanyike.Kwa mujibu wa takwimu shirika la Lufthansa huenda likapata hasara ya kiasi cha euro milioni 100 fedha taslimu pamoja na pato la tiketi ambazo tayari zimeuzwa.Tukio hili huenda likaitia doa sifa ya kampuni ya Lufthansa.   

Uchumi wa Ujerumani umekuwa ukisuasua tangu mwishoni mwa mwaka uliopita jambo linalowatia wafanyakazi wasiwasi wa kuzipoteza nafasi zao za kazi.Wengi wao wanawataka waajiri wawahakikishie kuwa hilo halitotokea na endapo inakuwa hivyo basi wapate fidia.Kampuni ya magari ya Volkswagen imelazimika kuchukua msimamo huo kwa sasa.Wafanyakazi wa makampuni mengine ya uhandisi wameridhia nyongeza ndogo za mishahara ili kuisawazisha hali.

Mgomo huo umezikwamisha shughuli zaidi katika uwanja wa ndege wa Frankfurt ulio mkubwa zaidi hapa Ujerumani.Hali ilikuwa hiyohiyo katika viwanja vya ndege vya miji ya Hamburg,Munich,Berlin na Dusseldorf.Mgomo huo umepangwa kuendelea hadi Alhamisi usiku.

Marubani hao wanadai nyongeza ya mishahara ya asilimia 6.4,ahadi ya kutofutwa kazi pamoja na nafasi hizo kuhamishiwa mataifa mengine ili kubana matumizi.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-RTRE/DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed