1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LUSAKA: Mkutano wa SADC wamalizika leo

17 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBYI

Viongozi wa jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, wamezindua kikosi maalum cha ulinzi kitakachosaidia juhudi za kulinda amani katika kanda hiyo.

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa SADC mjini Lusaka, mwenyekiti mpya wa jumuiya ya SADC, rais Levy Mwanawasa wa Zambia, amesema kikosi hicho kipya kitakuwa sehemu ya kikosi kikubwa cha Afrika, kitakachokuwa kikipelekwa kwa dharura kukabiliana na machafuko katika maeneo ya mizozo, kulinda amani, juhudi za kutoa misaada ya kiutu na kukabiliana na majanga asili katika maeneo yote barani Afrika.

Nchi zote wanachama wa SADC isipokuwa Madagascar, zimeahidi kutoa wanajeshi katika kikosi hicho.

Wakati huo huo, msemaji wa chama cha kiliberali cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini, Tony Leon, amesema jinsi viongozi wa jumuiya ya SADC walivyomshangilia rais Robert Mugabe katika mkutano wa mjini Lusaka, inadhihirisha kutokuwepo kwa ari ya kisiasa kuutanzua mgogoro wa Zimbabwe kati ya chama tawala cha ZANU-PF na chama cha upinzani, Movement for Democratic Change, MDC.