1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 sasa waondoka Goma

28 Novemba 2012

Kufuatia juhudi za kimataifa na mataifa jirani, hatimaye waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekubali kuondoka Goma na sasa wanakwenda kujikusanya kwenye mji wa Sake, nje kidogo ya Goma.

https://p.dw.com/p/16qzJ
Waasi wa M23 waondoka mji wa Goma.
Waasi wa M23 waondoka mji wa Goma.Picha: dapd

Akizungumza na DW, msemaji wa wapiganaji wa M23, Kanali Kazarama Vianeyi alisema tayari wanaanza kuwaondoa wapiganaji wao katika wilaya ya Masisi, na kuwapeleka katika mji wa Sake ulioko kilomita 27 kusini magharibi mwa mji wa Goma.


Akijibu swali kuhusu ni lini wataanza kuwaondoa Goma wapiganaji wao, kanal Vianey Kazarama alisema kujiondoa huko kutafanyika hatua kwa hatua.


Wakaazi wa mji wa Goma wameiambia DW kuwa usiku wa kuamkia leo waliyaona magari ya wapiganaji wa M23 pamoja na vifaa vya kivita bila yakujua wanaelekea wapi.


Mbinyo wa kimataifa?

Kuondoka Goma kwa wapiganaji wa M23 kunatokea kabla ya mkutano wa wakuu wa majeshi ya Kanda ya Maziwa Makuu utakaofanyika hapo Ijumaa mjini Goma. Baadhi ya wakaazi wa Goma wamewaomba viongozi wa nchi za Maziwa Makuu kuwalazimisha waasi wa M23 kuondoka kabisa kwenye mji wao.

Kiongozi wa tawi la kisiasa la M23, Askofu Jean Marie Runiga.
Kiongozi wa tawi la kisiasa la M23, Askofu Jean Marie Runiga.Picha: Michele Sibiloni/AFP/GettyImages

Bado si wazi ikiwa mbinyo wa jumuiya ya kimataifa na mataifa jirani ndio uliowasukuma waasi nje ya mji wa Goma, licha ya hapo awali kusema kwamba wasingelifanya hivyo hadi masharti yao kutimizwa, likiwemo la kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na utawala wa Rais Joseph Kabila.


Wiki moja ya kutekwa kwa mji wa Goma na waasi wa M23 kulipelekea huduma nyingi za kijamii kusita au kudumaa, zikiwemo zile za kifedha, ambapo mabenki kadhaa yalifungwa, na hivyo kuathiri hali ya maisha ya wakaazi, ambao tayari wako kwenye wakati mgumu sana.

Ndani ya kipindi hicho cha wiki moja, wakaazi wa Goma wamekuwa hawajui hasa ni nani viongozi wa jimbo na mji wao. Na hadi sasa hawajui utawala utabaki katika mikono ya nani, kati ya waasi wa M23 na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ripoti: John Kanyunyu/DW Goma
Mhariri: Mohammed Khelef