1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 wafanya ukatili dhidi ya ubinaadamu - HRW

11 Septemba 2012

Human Rights Watch imetoa taarifa inayoonesha kuwa waasi wa kundi la M23 la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamehusika katika ukatili na uhalifu wa kivita dhidi ya ya wanawake na watoto.

https://p.dw.com/p/166qN
Mwanajeshi wa Kongo akilinda doria mashariki mwa nchi hiyo.
Mwanajeshi wa Kongo akilinda doria mashariki mwa nchi hiyo.Picha: Reuters

Utafiti uliofanywa na Human Rights Watch kati ya Mei hadi mwanzoni wa Septemba kupitia kwa raia 190 wa Congo na Rwanda,wakiwemo waathirika wa matukio hayo,watu walioshuhudia, mamlaka za jamii na wapiganaji wa zamani wa kundi la M23 umethibitisha kuwa kundi hilo limetekeleza uasi huo.

Mkuu wa kitengo cha utafiti cha Human Rights Watch kwa kanda ya Afrika, Anneke Van Woudenberg, amesema kundi la M23 limekuwa likifanya unyama wa kutisha huko mashariki mwa Kongo, na kuihuisha serikali ya Rwanda ambayo amesema viongozi wake ni lazima wawajibike na unyama uliofanywa na kundi hilo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Human Rights Watch limekusanya visa 137 vya kufanyishwa kazi kwa nguvu wanaume na watoto katika kitongoji cha Rutshuru mashariki ya Kongo mnamo mwezi Julai, huku wengi wa watu hao wakitekwa nyara kutoka kwenye nyumba zao, mashambani, sokoni au wakati wakielekea kwenye mifugo yao, ambapo 15 kati yao wakiwa watoto.

Watu walioshudia matukio yaliyofanywa na kundi hilo waliliambia shirika hilo kuwa watu 33 waliajiriwa kwa nguvu na kundi la M23 na waliokataa waliadhibiwa na kufungwa kamba mikononi na miguuni na kisha kuuawa mbele ya wenzao.

Ukatili wa M23

Wakati tukiwa kwenye kundi la M23 hatukuwa na uamuzi na tulilazimika kubaki kwao au kuuawa. Wengi walijaribu kutoroka lakini walikamatwa na kuuawa," alisema kijana mmoja akilieleza shirika hilo.

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo.Picha: dapd

Human Rights Watch inakadiria kuwa kiasi cha vijana 600 wakiwemo pia watoto wameajiriwa kwa nguvu na kinyume na sheria nchini Rwanda ili wajiunge na kundi la M23 huko mashariki ya Kongo.

"Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halina budi kuweka vikwazo kwa kundi la M23 pia kwa viongozi wa Rwanda wanaowasaidia waasi hao kuendeleza unyama na ukiukaji wa haki za binadamu, mbali na Serikali ya Rwanda kukataa mara kadhaa kulisaidia kundi hilo," amesema Van Woudenberg.

Aidha Human Rights Watch linasema kuanzia mwezi Juni kundi la M23 limewauwa kiasi cha raia 15 wanaopinga vitendo vya kundi hilo katika maeneo wanayoyashikilia, na waasi hao kuendeleza vitendo vya ubakaji wa wanawake na wasichana 46 akiwemo msichana wa miaka minane.

Viongozi wakuu wa M23 wahusishwa

Shirika hilo pia limeainisha viongozi watano wa kundi la M23 wanaoongoza kwa vitendo vya unyanyasaji na ubakaji akiwemo kiongozi mkuu wa kundi hilo, Jenerali Bosco Ntaganda, anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa ukatili wa kivita na ukatili dhidi ya binadamu katika wilaya ya Ituri pamoja na Kanali Sultani Makenga anayejihusisha na kuwaajiri watoto na mauaji ya halaiki Mashariki ya Kongo.

Wanajeshi wa Kongo katika operesheni ya kumsaka Jenerali Bosco Ntaganda.
Wanajeshi wa Kongo katika operesheni ya kumsaka Jenerali Bosco Ntaganda.Picha: dapd

Kundi la Wataalamu na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa lililochungüza matumizi ya silaha limeeleza katika ripoti yake ya kurasa 48 ya Juni mwaka huu, haja ya kuwekewa vikwazo kwa serikali ya Kongo na kuhusika kwa Rwanda katika kulisaidia kundi la M23. Hata hivyo, Rwanda imeipinga ripoti hiyo.

Kundi hilo la Umoja wa Mataifa pamoja na Human Rights Watch yanamtaja Kanali Makenga kuwa ndiye muhusika katika kuwaajiri kwa nguvu watoto, mauaji ya halaiki, kuadhibu na ubakaji katika vijiji vya Kiwanja, Shalio na Buramba, huku kanali Baoudouin Ngaruye akiongozana naye katika mauaji ya Shalio.

Mgogoro wa kivita na matumizi ya silaha na ubakaji dhidi ya raia wasio na hatia yanayoendelea mashariki ya Kongo ni kinyume cha Ibara ya tatu ya Mkataba wa mwaka 1949 wa Geneva unaopinga vitendo vyote vya ubakaji, ajira za kulazimisha na vitendo vyote vya unyanyasaji.

Mwandishi: Khatib Mjaja/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef