1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafa jimboni Texas baada ya mripuko kiwandani

Admin.WagnerD18 Aprili 2013

Mripuko mkubwa uliotokea kwenye kiwanda cha mbolea karibu na mji wa Waco katika jimbo la Texas nchini Marekani, umewajeruhi watu wapatao 200 na kuuwa wengine ambao bado idadi yao haijatajwa.

https://p.dw.com/p/18IbA
Mabaki ya kiwanda cha mbolea kilichokumbwa na mripuko
Mabaki ya kiwanda cha mbolea kilichokumbwa na mripukoPicha: Reuters

Kiwanda cha kutengeneza mbolea kilichojengwa katika mji wa West ulioko umbali wa kilomita 130 kusini mwa jiji la Dallas kiliripuka na kuwaka moto saa moja usiku kwa saa ya mahali hapo, na sauti ya mripuko huo iliweza kisikika kutoka umbali wa km 45.

Akizungumza baadaye usiku, msemaji wa idara ya usalama wa raia katika jimbo la Texas amethibitisha kuwa watu kadhaa wameuawa katika mripuko huo, ingawa hakutaja idadi yao. Msemaji huyo ameongeza kuwa itachukua muda mrefu kabla ya kujua bayana kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mripuko huo.

Vifo vyaripotiwa

Hata hivyo, mbunge anayewakilisha eneo hilo Bill Flores amesema kuwa mripuko huo umetokea pale wazima moto walipokuwa wakijaribu kuzima moto uliokuwa umezuka katika sehemu moja ya kiwanda hicho. Kituo cha Televisheni cha CNN cha huko Marekani kimewanukuu maafisa wa afya wakisema kwamba watu wawili walikuwa wamekufa.

Baadhi ya waathiriwa wakipewa msaada wa uokozi
Baadhi ya waathiriwa wakipewa msaada wa uokoziPicha: picture-alliance/AP Photo

Gavana wa jimbo la Texas Rick Perry amesema maafisa wa jimbo lake wanaifuatilia hali kwa makini. Aidha, gavana huyo ameongeza kuwa ofisi yake inatoa msaada wa hali na mali kwa mamlaka ya eneo lililoathiriwa, na kutoa pole kwa wale waliofikwa na maafa.

Kama filamu ya kutisha

Watu walioshuhudia mripuko huo ukitokea wamesema kwamba ulitoa sura ya filamu za kutisha. Wengine wameilinganisha hali hiyo na ile ya wakati wa vita vya Iraq.

Walioshuhudia waliinganisha hali ya mripuko huo na filamu za kutisha
Walioshuhudia waliinganisha hali ya mripuko huo na filamu za kutishaPicha: picture-alliance/AP Photo

Moto uliotokana na mripuko huo umeenea katika mtaa mzima, na miongoni mwa nyumba zilizoathirika ni makazi ya wazee. Baadhi ya wazee waliohamishwa kutoka nyumba hiyo walionekana wakipatiwa matibabu katika kituo cha afya.

Vituo vya matibabu ya dharura vimewekwa karibu, na wakazi wameamriwa kwenda mbali kwa hofu kwamba moto unaowaka unaweza kusambaza moshi wenye sumu. Hospitali inayoendeshwa na kanisa la Kibaptisti katika mji wa Waco imeripoti kupokea majeruhi 66,  miongoni mwao wakiwa 38 walio katika hali mahututi.

Viwango duni

Afisa wa polisi katika mji wa Waco sajenti William Patrick Swanton amewaambia waandishi wa habari kwamba hana maelezo kamili kuhusu idadi ya watu wanaofanya kazi katika kiwanda cha mbolea kilichoripuka. Kiwanda hicho kilitajwa katika ripoti ya tume ya viwango na mazingira ya jimbo la Texas mwaka 2006, ambayo ilisema hakitimizi wiwango vya kupewa leseni ya kufanya kazi.

Uchunguzi wa tume hiyo ulifanywa baada ya kupata malalamiko ya kuwepo kwa harufu kali ya kemikali ya ammonia katika kiwanda hicho.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/DPA

Mhariri:Abdul-Rahman