1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano dhidi ya Hosni Mubarak yanaendelea kwa siku ya 18

11 Februari 2011

Maelfu ya watu wamekusanyika katika uwanja wa Al-Tahrir, tayari kushiriki katika maandamano makubwa kabisa -baada ya sala ya ijumaa.Wanajeshi kwa upande wao wametangaza taarifa muhimu kuhusu hali nchini Misri.

https://p.dw.com/p/10FcE
Rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: AP

Waaandamanaji wamekesha usiku kucha katika uwanja wa al-Tahrir na tangu alfajiri wameanza kujiandaa kwa maandamano makubwa dhidi ya rais Hosni Mubarab asiyetaka kung'oka madarakani.

Katika wakati ambapo baadhi yao walikuwa bado wamejinyosha katika uwanja huo uliogeuka kuwa kitambulisho cha vuguvugu la malalamiko yasiyokuwa na mfano,wengine tayari wanalalamika na kupaza sauti dhidi ya rais Mubarak huku wakipepea bendera za Misri.

Kundi dogo la waandamanaji limeongozana hadi karibu na kasri la rais Mubarak wakipiga makelele "Atoweke Mubarak.Bango moja lililoandikwa matamshi hayo hayo wamelitundika juu ya senyenge inayozunguka lango la kuingilia katika kasri hilo.

NO FLASH Ägypten Kaior Proteste
Waandamanaji wamezidi uchunguPicha: ap

Waandamanaji wameghadhibika kutokana na hotuba ya jana ya rais Hosni Mubarak aliyesema anamkabidhi baadhi tu ya madaraka yake makamo wa rais Omar Suleiman, lakini ataendelea kuwepo madarakani hadi September, na kuapa atakufa huko huko nchini Msri.

Ghadhabu hazijapungua,viatu vinaendelea kuvurumishwa katika picha za rais huyo, na wengine wakidai :

"Nnataka waliohusika na kuuliwa vijana na mashahidi waadhibiwe.

Kamanda mmoja wa kijeshi aliyejiunga na waandamanaji katika uwanja wa al-Tahrir amesema maafisa wengine kama 15 hivi wenye vyeo vya kuanzia kepteni hadi luteni kanali wamejiunga pia na waandamanaji.

"Vuguvugu la mshikamano wa wanajeshi kwa umma wa Misri limeshaanza" amesema hayo kamanda Ahmed Ali Shouman baada ya sala ya alfajiri hii leo.

Omar Suleiman Vizepräsident von Ägypten
Makamo wa rais Omar SuleimanPicha: AP

Baraza kuu la kijeshi limetangaza taarifa muhimu hivi punde kuhusu hali namna ilivyo nchini Misri.Wamewataka wananchi warejee katika shughuli zao za kawaida ,wameahidi kudhamini mageuzi yaliyoahidiwa na Rais Hosni Mubarak, na wameahidi vilevile kuondoa sheria ya hali ya hatari.

Baraza hilo limekutana tena leo asubuhi na kuongozwa na waziri wa ulinzi, Hussein Taantawi.

Katika kikao chake cha kwanza hapo jana, baraza kuu la wanajeshi lililisema linatathmini hatua zinazohitajika ili kuihifadhi nchi na kuunga mkono madai ya haki ya wananchi.

Mwandishi Hamidou Oummilkhheir,afp,reuters,dpa

Mpitiaji: Miraji Othman