1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano dhidi ya Serikali yachacha Moldova

8 Aprili 2009

Polisi wadhibiti majengo ya bunge na kuwakamata waandamanaji kadhaa katika ghasia Moldova

https://p.dw.com/p/HSkF
Waandamanaji wateketeza moto mabango ya chama cha kikomunisti,MoldovaPicha: picture-alliance/ dpa

Polisi wameyadhibiti majengo ya bunge mapema hii leo na kuwakamata waandamanaji kadhaa waliokuwa wamebakia katika eneo hilo kabla ya kuwafurusha wengine waliokuwa katika uwanja ulioko mbele ya majengo ya bunge.

Hata hivyo waandamanaji ambao wamechochewa na wanaharakati vijana na sio makundi ya kisiasa yanayotambulika wameapa kuendelea na maandamano hayo hadi matokeo hayo ya uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki yatakapobatilishwa.


Vijana wanaoshiriki maandamano hayo wanadai wamepoteza subira na serikali na wanachokitaka ni hali bora ya maisha.Kijana Sergei mwenye umri wa miaka 22 akishiriki maandamano hayo kuelekea bunge amesema hatua wanaoyoichukua ya kuandamana sio hatua nzuri lakini hakuna njia nyingine ya kupambana na ukomunisti katika eneo hilo.


Waandamanaji wanalalamika juu ya hali mbaya ya kiuchumi ambayo imeifanya Moldova kuwa nchi maskini kabisa barani Ulaya.Kiongozi wa upinzani nchini humo amesema kwamba maafisa wa tume ya uchaguzi wamekataa kukubali ombi lao la kutaka kura zihesabiwe upya.


Moldau Unruhen in Chisinau Wahlleiter Eugeniu Stirbu
Mkuu wa tume ya uchaguzi Eugeniu Stirbu, alaumiwa na upinzani kwa kukataa marudio ya kuhesabu kura.Picha: AP

Vlad Filat anasema tume kuu ya uchaguzi imevunja makubaliano ambayo chama chao ilifikia na rais wa nchi hiyo Vladmir Voronin.Kiongozi huyo wa upinzani wa chama cha Liberal Demokcratic amaefahamisha hii leo kwamba kutokana na maandamano ya wafuasi wake huenda serikali ikachukua hatua kali dhidi ya viongozi wa kisiasa pamoja na walioshiriki katika maandamano hayo.Maandamano zaidi yanatazamiwa kufanyika baadae leo hii.


Katika kipindi cha siku mbili zilizopita zaidi ya watu 15000 walishiriki hali ambayo pia haikutarajiwa na wapinzani. Vlad Filat kiongozi wa chama cha Liberal Demokratic anasema wamejaribu kuituliza hali ya mambo ili kuzuia maandamano kuenea kutokana na hofu kwamba huenda wanasiasa wa upinzani wakakamatawa lakini wameshindwa kuyazuia kwasababu watu wa nchi hiyo wamechoka kuishi kwa uhuru na bila ya kuhofia kitu.Chama tawala cha kikomunisti cha rais Voronin cha PCRM kilishinda asilimia 50 ya kura katika uchaguzi wa bunge ambao kwa mujibu wa waangalizi wa nchi za magharibi ulizingatia kwa kiasi kikubwa viwango vya kimataifa.Ushindi huo unamaanisha unatoa nafasi ya kutosha kwa chama hicho kumchagua mrithi wa rais Voronin hali ambayo inawakasirisha waandamanaji.


Kiasi cha watu 100 walijeruhiwa katika ghasia hizo wakiwemo maafisa wa polisi.Rais wa serikali ya kikomunisti Vladmir Voronin ambaye amekuwa mtu mwenye usemi mkubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 8 na anayetazamiwa kuondoka madarakani baada ya kuongoza kwa mihula miwili mfululizo amewaonya waandamanaji kwamba serikali itachukua hatua kali dhidi yao.


Jumuiya ya kimataifa imetoa mwito wa utulivu katika nchi hiyo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon amezitaka pande zote kujizuia na ghasia huku mkuu wa sera za nje katika Umoja wa Ulaya Javier Solana akisema ghasia hizo dhidi ya serikali ni hatua isiyokubalika.Rais wa Urusi Dmitry Medvedev hapo jana alifanya mazungumzo na mwenzake wa Moldova kwa njia ya simu na kumtaka atafute haraka azimio la amani katika mzozo huo.


Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman