1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano Hamburg kabla ya mkutano wa G20

Sekione Kitojo
3 Julai 2017

Wakati wanaharakati wanaopinga utandawazi wakiingia mitaani mjini Hamburg kabla ya mkutano wa kilele wiki hii wa G20, kansela  Angela Merkel alisema viongozi watalazimika kuangalia ukuaji endelevu na unaoijumuisha jamii.

https://p.dw.com/p/2fotj
Protestwelle gegen den G20 Gipfel
Picha: picture-alliance/dpa/M. Scholz

Katika  hotuba  yake ya  kila  wiki, Merkel alisema  mkutano wa  kilele  mwaka  huu  wa  G20  utaangalia  masuala yanayopigiwa  upatu  na  waandamanaji  kama  kugawana utajiri  na  matumizi ya  rasilmali, pamoja  na  masuala mengine  yanayokaribiana kama  mabadiliko  ya  tabia nchi, masoko  huru, ulinzi  wa  watumiaji  bidhaa  na kulinda  viwango  vya kijamii.

Hamburg G20 Protest-Camp in Entenwerder
Polisi na waandamanaji wakipambana wakati polisi walipoondoa kambi ya waandamanaji ya mahema mjini Hamburg(02.07.2017)Picha: picture-alliance/dpa/B. Marks

Polisi  mjini  Hamburg  imesema  waandamanaji  10,000 waliandamana  kwa  amani  katika  mvua  mjini  humo  jana Jumapili  ikiwa  ni  hatua  ya  mwanzo  kabla  ya  mkutano huo  utakaofanyika  kuanzia  Julai 7-8, ambapo polisi 21,000 kutoka  sehemu  mbali  mbali  nchini  Ujerumani watakuwa  na  jukumu  la  kuweka  ulinzi  kwa  ajili  ya mkutano  huo  wa mataifa  20 yenye  uchumi  mkubwa duniani.

Yalikuwa  maandamano  ya  kwanza  kati  ya  maandamano 30  yaliyoorodheshwa  kufanyika  wiki  hii. Baadhi  ya waandamanaji  walibeba mabango  yanayosomeka "Pambana  na  umasikini", "zuia makaa ya  mawe" na "sayari ya dunia kwanza".

Baadhi  ya  waandamanaji walizungumza  na  vyombo  vya habari  na  kutoa  mawazo  yao.

"Ni juu ya kuwa  na  dunia  kwa  ajili  ya hapo  baadaye. Tuna watoto na inapaswa kuwa dunia nzuri kwake, pia."

"Uchumi ndio  msingi wa  maisha  ya  watu, na  kunapaswa kuwa  na  haki  zaidi  ndani  yake."

Protestwelle gegen den G20 Gipfel
Maandamano ya walinzi wa mazingira katika mkutano wa kilele wa G20 mjini HamburgPicha: picture-alliance/dpa/A. Heimken

Wasi wasi wa  kuzuka ghasia

Maafisa  nchini  Ujerumani  wanajitayarisha  kwa  ghasia zaidi, wakihofia  kuwa  maandamano  yanaweza  kugeuka kuwa  ya  ghasia  kama  ilivyokuwa  nje  ya  mkutano  wa kilele  wa  mataifa  yenye  utajiri  wa  viwanda G8, mjini Genoa, nchini  Italia  mwaka  2001 wakati  mtu  mmoja alipigwa  risasi na  mamia  walijeruhiwa.

Merkel  akiwania  muhula  wa  nne  madarakani  katika uchaguzi  utakaofanyika  Septemba  24  mwaka  huu, ameainisha  masuala  kama  hivi: "Nini tunakifanya kuhusiana  na  maliasili  yetu?  Ni utaratibu  gani wa kugawana  utajiri? Watu  wangapi  wanashiriki? na  nchi ngapi zina uwezo wa  kufaidika kutokana  na  hayo?

G20-Kunst in Hamburg
Sanaa mjini Hamburg zikionesha watu ambao hawana la kufanya katika dunia iliyochafukaPicha: DW/A. Drechsel

Bila  ya  kutaja  waandamanaji  ambao maafisa  wa  polisi nchini  Ujerumani  wana  wasiwasi  juu  ya  uwezekano  wa vitendo  vya  uharibifu  wiki  hii  katika  mji  wa  pili  kwa mkubwa  nchini  Ujerumani, Merkel amedokeza  kwamba masuala  haya  ambayo  si  ya  kawaida  yamelazimishwa kuingia  katika ajenda  ya  mkutano  wa G20.

Katika  hotuba  bungeni  wiki iliyopita, Merkel  aliahidi kupambana  kwa  ajili  ya  biashara  huru na  kusukuma juhudi  za kimataifa  kupambana  na  mabadiliko  ya  tabia nchi  katika  mkutano  huo, akipambana  na  sera  za "Marekani  kwanza" za  rais  wa  Marekani  Donald Trump. Mkutano wa  G20  unafuatia  mkutano  wa  G7 mjini  Sicily, Italia  mwezi  mmoja  uliopita  ambao  uliweka wazi tofauti kubwa  baina  ya  mataifa  mengine  ya  magharibi na Trump  kuhusiana  na  mabadiliko  ya  tabia  nchi, biashara na uhamiaji. Trump  baadaye  alitangaza  kwamba  anaitoa nchi  yake  katika  makubaliano  muhimu  ya  kupambana na  mabadiliko  ya   tabia  nchi  yaliyofikiwa  mwaka  2015 mjini  Paris.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Josephat Charo