1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano kuhimiza uvumilivu

13 Januari 2015

Kansela Angela Merkel na Rais Joachim Gauck wa Ujerumani Jumanne (13.01.2014) wanashiriki maandamano ya kutetea uvumilivu katika jamii na kupinga vuguvugu la maandamano linalozidi kukua dhidi ya Uislamu nchini.

https://p.dw.com/p/1EJbV
Ishara ya Uislamu nchini Ujerumani.
Ishara ya Uislamu nchini Ujerumani.Picha: picture-alliance/Frank Rumpenhorst

Kansela Angela Merkel na Rais Joachim Gauck wa Ujerumani Jumanne (13.01.2014) wanashiriki katika maandamano ya kutetea uvumilivu katika jamii na kupinga vuguvugu la maandamano linalozidi kukua dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani.

Mbali na Rais Gauck ambaye atayahutubia maandamano hayo yatakayofanyika jioni ya leo katika eneo la kihistoria la Lango la Brandeburg katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin mawaziri wengi wa serikali ya Merkel pia wanatarajiwa kuhuhudhuria.

Hapo jana Merkel alisisitiza kwamba Uislamu ni sehemu ya Ujerumani yeye pamoja na Rais Gauck wamelishutumu kundi la Wazalendo wa Ulaya dhidi ya Kusilimishwa kwa Ulaya PEGIDA kwa kutaka kuigawa jamii ya Ujerumani na kufanya hivyo kwa kutumia vibaya kwa faida yao hufo walio nayo wananchi katika suala la uhamiaji,ugaidi na Waislamu wa itikadi kali.

Maandamano hayo ya leo yanakusudia kujibu yale yanayofanyika kila wiki katika mji wa mashariki wa Ujerumani wa Dresden yanayoandaliwa na kundi la PEGIDA ambapo Jumatatu yalihudhuriwa na watu 25,000 huku maandamano dhidi ya kundi hilo nayo yakifanyika nchi nzima na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 100,000.

Ujumbe wa amani na uvumilivu

Wakiyatangaza maandamano hayo ya Jumanne Baraza la Waislamu nchini Ujerumani na Jumuiya ya Waturuki mjini Berlin zimesema Waislamu nchini Ujerumani wanalaani kwa nguvu zote mashambulizi ya kigaidi ya kuchukiza yaliotokea nchini Ufaransa na kwamba wanataka kuonyesha mshikamano wao na wahanga wa Ufaransa.

Waislamu wakiwa katika ibada ya sala ya Ijumaa mjini Berlin.
Waislamu wakiwa katika ibada ya sala ya Ijumaa mjini Berlin.Picha: Reuters/Hannibal

Zimesema kwa kutumia maandamano hayo wanataka kutuma ujumbe wa amani na uvumilivu,ujumbe dhidi ya chuki na matumizi ya nguvu kwa ajili ya Ujerumani yenye mchanganyiko wa watu ambayo inaheshimu na kulinda uhuru wa kujieleza na dini.

Katika maoni ya mtandaoni ya gazeti mashuhuri la Spiegel nchini Ujerumani Kansela Merkel amepongezwa kwa kutocheza mchezo wa ghilba ambapo katika hotuba yake ya mwaka mpya alikuwa mstari wa mbele wa kupinga vuguvugu la PEGIDA kwa kuwalaani viongozi wa kundi hilo kwa kuwa watu wasiopenda maangiliano na hata waliojaa chuki nyoyoni.Ameonyesha msimamo wa wazi wa unaostahiki kutukuzwa wa kupinga chuki dhidi ya Uislamu.

Vuguvugu la PEGIDA

Maandamano ya PEGIDA na mengine madogo kama hayo yamechochewa na kile kinachoelezwa kuwa ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi nwanaotafuta hifadhi ya kisiasa nchini jambo lililoifanya serikali kuhangaika kuwatafutia makaazi katika majengo ya shule,maofisi na kuwaweka pia katika makontena vijijini.

Maandamano ya PEGIDA dhidi ya Uislamu mjini Dresden. (13.01.2014)
Maandamano ya PEGIDA dhidi ya Uislamu mjini Dresden. (13.01.2014)Picha: Reuters/F. Bensch

Mwaka jana Ujerumani ilipokea zaidi ya maombi 180,000 ya watu wanaotaka hifadhi likiwa ni ongezeko la asilimia 57 kutoka mwaka 2013 na wengi wao walikuwa wanatokea Syria,Afghanistan, Iraq,Eritrea na Somalia na pia kutoka nchi kadhaa za Balkan.

Ujerumani ina takriban wakaazi milioni nne wa Kiislamu sawa na kama asilimia tano ya wananchi wake milioni themanini.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP /AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-rahman