1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaCuba

Maandamano kutaka umeme na chakula nchini Cuba

Saleh Mwanamilongo
18 Machi 2024

Serikali imeonya dhidi ya wale iliowaita kuwa magaidi walioko Marekani na maadui wa Mapinduzi ambao wanatumia wimbi la hasira za wananchi dhidi ya kukatika kwa umeme na uhaba wa chakula nchini humo.

https://p.dw.com/p/4ds5a
Mamia ya waandamanai walijitokeza huko Santiago de Cuba kutaka umeme na chakula
Mamia ya waandamanai walijitokeza huko Santiago de Cuba kutaka umeme na chakulaPicha: Yamil Lage/AFP

Kwenye ujumbe kupitia mtandao wa X, Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alihimiza mazungumzo na waandamaji katika mazingira ya utulivu. Diaz alikiri kwamba watu kadhaa wameelezea kutoridhishwa kwao na ukosefu wa umeme na usambazaji wa chakula nchini, huku akionya kuwa maadui wa Mapinduzi ya Cuba ndio wanalenga kutumia hali hiyo. Rais Diaz aliwanyoshea kidole cha lawama wapinzani walioko nchini Marekani.

Kwa upande wake, Ubalozi wa Marekani mjini Havana uliitaka serikali ya Cuba kuheshimu haki za waandamanaji. Bila kusita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodriguez aliitaka Washington kutoingilia masuala ya ndani ya nchi yake.

Kwenye mitandao ya kijamii picha za maandamano huko Santiago de Cuba, na vile vile huko Bayamo, katika jimbo jirani la Granma, zilichapishwa . Mkaazi mmoja wa mji wa Santiago de Cuba wenye wakazi zaidi ya nusu milioni alisema waandamanaji walikuwa wakipiga kelele kuomba chakula na umeme.

Kijana huyo alithibitisha kwa waandishi habari kwamba umeme ulirudi baadaye mchana na malori mawili ya mchele yalipelekwa kwenye eneo hilo. Kulingana na mashahidi kadhaa huduma za mtandao zilisitishwa jijini humo.

Kukatika kwa umeme kwa muda mrefu na uhaba wa chakula vimekuwa kero kwa wananchi wa Cuba. Na kusababisha maandamano ya mitaani kulalamikia ughali wa maisha.

Cuba yapitia wakati mgumu wa kiuchumi

Mwishoni mwa wiki iliopita tatizo lilichangiwa na uhaba wa mafuta ulioathiri nchi nzima
Mwishoni mwa wiki iliopita tatizo lilichangiwa na uhaba wa mafuta ulioathiri nchi nzimaPicha: Delil Souleiman/AFP/Getty Images

Askofu Mkuu wa jiji la Santiago de Cuba, Dionisio García alisema hali kwa sasa ni ngumu kutokana na ukosefu wa umeme, lakini wanamatumaini kwamba suluhisho la mzozo huo litapatikana.

Tangu mwanzoni mwa Machi, Cuba imekuwa ikikabiliwa na wimbi jipya la ukosefu wa umeme kutona na kazi za ukarabati wa bwawa kuu la umeme kisiwani humo.

Mwishoni mwa wiki iliopita tatizo lilichangiwa na uhaba wa mafuta ulioathiri nchi nzima. Mamlaka ilisema Kisiwa kizima cha Cuba kiliathiriwa na kukatika kwa umeme ikiwa ni pamoja na mji mkuu Havana. Uchumi wa kisiwa hicho chenye wakaazi milioni 11 umeshindwa kuimarika tangu janga la corona la mwaka 2020 na vikwazo vya Marekani toka 1962.

Maandamano ya Jumapili ni makubwa zaidi tangu yale ya 2022 wakati kisiwa hicho kilikumbwa na kukatika kwa umeme kila siku, hali ambayo tayari ilikuwa imechochea maandamano katika majimbo kadhaa na vile vile huko Havana.

Chanzo : AFP