1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa Ufaransa

Hamidou, Oumilkher22 Mei 2008

Wafaransa wateremka majiani kuishinikiza serikali iregeze kamba katika suala la malipo ya uzeeni

https://p.dw.com/p/E4OT
Mgomo wa shirika la usafiri SNCFPicha: picture-alliance / maxppp


Maelfu ya wafaransa wameanza kuteremka majiani katika kila pembe ya nchi hiyo wakijibu mwito wa vyama vinane vya wafanyakazi vinavyoitaka serikali ya rais Nicolas Sarkozy irekebishe mswaada wa mageuzi ya malipo ya uzeeni.


Jumla ya maandamano mia moja yanafanyika katika kila pembe ya Ufaransa hii leo,vyama vya wafanyakazi vinataraji kuigeuza siku hii ya leo kua "siku ya kupimana nguvu ya waajiriwa wa sekta za serikali na za kibinafsi dhidi ya mageuzi ya malipo ya uzeeni.


Jean Marc Cannon ni mwanachama wa shirika la wafanyakazi serikalini CGT,anasema mgomo huu ni wa lazima katika kutetea masilahi jumla ya sekta ya jamii.


"Nnaona ni sawa kimsingi kwamba kila mmoja katika idara za serikali na huduma za jamii anapania kupigania maendeleo ya kijamii mkwa wote.Maandamano haya ni ya mchanganyiko kwasababu tunataka kutetea masilahi jumla ya jamii."


Siku hii ya leo inashuhudia pia migomo katika sekta ya usafiri wa jamii ambapo shughuli za usafiri zimeparaganyika katika miji kadhaa ya mikoani ikiwa ni pamoja na mji mashuhuri wa kusini Marseille.Treni moja tuu kati ya mbili ndio inayofanyika kazi hii leo kote nchini Ufaransa.Lakini katika daraja ya kimataifa shughuli za usafiri wa ndege na treni zinaendelea kama kawaida.


Serikali ya rais Nicolas Sarkozy inang'ang'ania msimamo wake ule ule shupavu,hasa linapohusika suala la malipo ya uzeeni ambapo kuanzia mwakani serikali hiyo inawataka watu wafanye kazi kwa miaka 41 badala ya 40 ili kupata malipo kamili ya uzeeni.


Maandamano haya ya leo yanajiri baada ya maandamano ya wiki kadhaa ya wanafunzi wa shule za sekondari,maandamano ya waalimu na malalamiko ya wavuvi ambao baadhi yao wanaandamana pia hii leo licha ya ahadi ya serikali ya kutenga  misaada yenye thamani ya dala milioni 110 hadi mwisho wa mwaka huu.Wavuvi wanahisi msaada huo hautoshi.


Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya umma ulioongozwa na taasisi ya CSA na kuchapishwa na gazeti la Humanité hii leo,asili mia 60 ya wafaransa walioulizwa maoni yao wanaunga mkono migomo mbali mbali inayofanyika nchini humo.


Katibu mkuu wa shirika la CGT,Bernard Thibault anasema lengo sio kuwashawishi watu wote wagome,naiwe katika sekta ya usafiri au nyenginezo,lengo ni kuishinikiza serikali ibadilishe msimamo wake."


Jana usiku waziri mkuu Francois Fillon amedhibitisha mipango ya serikali ya kurefusha muda wa kulipa kodi ya uzeeni kuanzia mwaka 2009,hatua kwa hatua hadi ifikapo mwaka 2012.Kwa mujibu wa serikali,uamuzi huo uliotajwa katika sheria iliyopitishwa mwaka 2003 ndio njia pekee ya maana ya kukidhi mahitaji ya fedha yanayotokana na kuongezeka kiwango cha maisha ya wafaransa.