1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano mapya yafanyika Misri

Admin.WagnerD27 Januari 2012

Maandamano makubwa yanafanyika katika medani ya Tahrir katika mji mkuu wa Misri Cairo, kushinikiza utawala wa mpito unaoongozwa na baraza la kijeshi kuharakisha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa viongozi wa kiraia.

https://p.dw.com/p/13reS
Medani ya Tahrir mjini Cairo imekuwa kitovu cha vuguvugu la mageuzi
Medani ya Tahrir mjini Cairo imekuwa kitovu cha vuguvugu la mageuziPicha: picture-alliance/dpa

Makundi ya upinzani yapatayo 60 nchini Misri yametangaza kwamba wafuasi wake watashiriki katika maandamano hayo baada ya sala ya mchana leo, wakati ambapo imani ya wananchi ikizidi kupungua juu ya matokeo ya vuguvugu la mageuzi lililomwondosha madarakani Rais Hosni Mubarak. Vikosi vya usalama vimeondolewa kwenye medani ya Tahrir kuepusha makabiliano na waandamanaji wenye hasira. Machafuko yenye umwagaji damu yameshuhudiwa mara kadhaa kwenye medani hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Upinzani nchini Misri umelikosoa Baraza la Kijeshi linaloongoza utawala wa mpito tangu kuangushwa kwa serikali ya Hosni Mubarak, ukilishutumu kukwamisha mageuzi na kuhusika na visa vya ukiukaji wa haki za binadamu. Maandamano ya leo ni hatua nyingine ya kuongeza mbinyo kwa baraza hilo liharakishe mchakato wa kurejesha madaraka mikononi mwa watawala wa kiraia.

Jana wanaharakati wa mageuzi walifanya maandamano kupinga jinsi mahakama inavyojivuta kuwahukumu maafisa wa serikali ya Rais Hosni Mubarak wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya waandamanaji takribani 800 mwaka jana. Ripoti za mashirika ya haki za binadamu zinasema waandamanaji wengine 90 wameuawa mnamo miezi ya hivi karibuni.

Mkuu wa Baraza la Kijeshi linaloongoza Misri Field Marshal Mohamed Hussein Tantawi
Mkuu wa Baraza la Kijeshi linaloongoza Misri Field Marshal Mohamed Hussein TantawiPicha: picture-alliance/dpa

Huku hayo yakiarifiwa, Misri imewazuia raia 10 kutoka Ulaya na Marekani kuondoka ndani ya nchi hiyo ikiwahusisha na kuchechea maandamano. Miongoni mwa waliozuiliwa ni mtoto wa Waziri wa Usafiri wa Marekani, Ray LaHood. Marekani imetoa onyo kwa Misri kwamba hatua hiyo inaweza kuathiri msaada wa kijeshi wa dola bilioni moja ambao Marekani huutoa kwa nchi hiyo kila mwaka.

Wapinzani wa Baraza la Kijeshi linaloongoza Misri wanasema majenerali katika baraza hilo wanataka kuichafua sura ya waandamanaji machoni mwa raia, na kunyamazisha mashirika ambayo yanaweza kuwa kizingiti kwenye udhibiti wao wa madaraka.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Victoria Nuland amesema kuwa wiki iliyopita, Rais Barack Obama wa Marekani aliongea na mkuu wa baraza hilo la kijeshi Field Marshal Hussein Tantawi, na kumkumbushia umuhimu wa mashirika hayo katika mchakato wa kidemokrasia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani Victoria Nuland
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani Victoria NulandPicha: AP

Onyo la Marekani kwa Misri limetolewa baada ya mkurugenzi wa shirika moja liitwalo International Republican Institute lenye makao yake mjini Washington, Sam LaHood, kuzuiliwa na maafisa wa uhamiaji kwenye Uwanja wa Ndege wa Cairo.

Shirika lake ni mojawapo ya mashirika kadhaa yaliyofanyiwa upekuzi mwezi uliopita. Mamlaka nchini Misri ilisema upekuzi huo ulikuwa utaratibu wa kawaida kuangalia kama mashirika hayo yalikuwa yakifanya kazi kihalali.

Seneta John McCain ambaye aligombea urais wa Marekani dhidi ya Rais Barack Obama, ameonya kuwa mwendendo wa utawala wa Misri kukandamiza makundi ya kiraia, unaweza kuzorotesha uhusiano baina yake na Marekani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPA/AP

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed