1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano Ukraine na Thailand Magazetini

Oumilkher Hamidou2 Desemba 2013

Maandamano nchini Ukraine,hali nchini Thailand na juhudi za kuwatanabahisha wafuasi wa chama cha Social Democratic SPD waunge mkono mkataba wa serikali ya muungano ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1ARav
Waandamanaji wamekusanyika licha ya avizuwizi barabarani mjini KievPicha: Reuters

Tunaanzia Ukraine ambako maandamano dhidi ya uamuzi wa rais Viktor Yanukowitsch wa kusitisha mazungumzo pamoja na Umoja wa Ulaya umezidisha ghadhabu za wale wanaopendelea kuiona nchi hiyo ya Ulaya ya Mashariki ikijiunga siku moja na Umoja wa Ulaya.Baada ya ishara za mwanzo mwanzo,Yanukowitsch amejikuta baadae akilazimika kubadilisha msimamao wake. Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten linatoa sababu ya hali hiyo na kuandika:"Ukraine haijimudu hata kidogo,mtu anaweza kusema takriban imefilisika.Haina hata upenu wa kufurukuta kisiasa nchi hiyo yenye wakaazi milioni 45 kwa sababu ya kuitegemea kwa kila hali Urusi.Vitisho vya kila mara vya Moscow vya kuiwekea vizuwizi vya kibiashara vinaonyesha kuleta tija.Benki za Urusi ndizo zinazotoa mikopo mikubwa mikubwa nchini humo ,wanajeshi wa Urusi wana kituo chao huko na gesi ya Urusi ndio uti wa mgongo wa Ukraine.Ndio maana kilio cha waandamanaji kimemlenga zaidi Putin na kibaraka wake Yanukowitsch.Hata hivyo wanatambua pia mara hii,mapambano yao wanayaendesha peke yao.

Kinyang'anyiro cha kuania Madaraka

Sawa na Ukraine ,maandamano yamepamba moto pia nchini Thailand ambako pia wafuasi wa upande wa upinzani wanadai serikali ijiuzulu.Gazeti la "Braunschweiger Zeitung" linaandika:Mtu angeweza kusema maandamano yamesababishwa na ghadhabu za umma-Lakini hilo si kweli.Maandamano hayo na matumizi ya nguvu yanachochewa na Suthep Thausuban-makamo wa zamani wa waziri mkuu anaeongoza hivi sasa chama cha upinzani cha Democratic.Suthep ndie anaepalilia mambo na kuchochea matumizi ya nguvu bila ya kujali kama maisha ya binaadam yanaangamia.Alifanya hivyo hivyo alipokuwa makamo waziri mkuu alipoamuru nguvu zitumike kuwatawanya waandamanaji.Miaka kadhaa iliyopita utawala wa kaka yake waziri mkuu Yingluck Shinawatra-Thaksin,nao pia ulitumia nguvu dhidi ya makundi ya kiislam,ulikuwa ukikosolewa kuhusika na rushwa na kutumia vibaya madaraka ya serikali.Kwa hivyo ni shida kuashiria upande upi unapigania zaidi masilahi ya wananchi.Kimoja ni dhahir:Waandamanaji mabarabarani na pengine wananchi wote kwa jumla wanatumiwa tu katika kinyang'anyiro hiki cha kuania madaraka.

Thailand Antiregierungsproteste in Bangkok 2. Dezember
Mpinzani wa serikali akivurumisha maguruneti dhidi ya polisiPicha: Reuters

Wana Social Democratic Watanabahi

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu juhudi za chama cha Social Democratic nchini Ujerumani kuwatanabahisha wanachama wake waunge mkono mkataba wa serikali ya muungano uliofikiwa pamoja na vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU.Gazeti la "Nordwest Zaitung" linaandika:"Hali imeanza kubadilika katika chama cha SPD kuelekea serikali ya muungano wa vyama vikuu.Ni kweli kwamba wasi wasi haujatoweka moja kwa moja katika mikutano inayoitishwa na SPD mikoani.Hata hivyo idadi kubwa ya wana Social Democratic wanaonyesha hivi sasa kuwaunga mkono viongozi wao.Hata katika ngome za chama hicho,wafuasi wamemshangiria mwenyekiti Sigmar Gabriel mwishoni mwa majadiliano yao.

SPD Regionalkonferenz 28.11.2013 Sigmar Gabriel
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akiwahutubia wanachama huko Hofheim katika juhudi za kuwatanabahisha waunge mkono mkataba wa serikali ya muunganoPicha: picture-alliance/dpa

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Gakuba Daniel