1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya Nairobi yaahirishwa hadi wiki ijayo

3 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CjtQ

NAIROBI

Chama kikuu cha upinzani nchini Kenya kimeahirisha maandamano makubwa yaliokuwa yamepangwa kufanyika leo hii katika mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi kupinga kuchaguliwa tena kwa Rais Mwai Kibaki baada ya polisi kutumia mabomu ya kutowa machozi na mabomba ya maji kutawanya mamia ya waandamanaji.

Hata hivyo maandamano mapya yamepangwa kufanyika Jumanne ijayo.Akizungumza na waadishi wa ahabari kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesisitiza kwamba ataendelea kupinga matokeo ya uchaguzi huo mkuu wa wiki iliopita.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika John Kufour ambaye ni Rais wa Ghana alikuwa anatazamiwa kuwasili nchini Kenya leo hii kusaidia kusuluhisha mzozo uliozuka baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300 nchini kote hata hivyo inaonekana kwamba kutokana na hali mbaya ya usalama ziara hiyo ya Kufour imefutwa.

Askofu Mkuu wa Kianglikana Desmond Tutu wa Afrika Kusini na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel yuko nchini Kenya kujaribu kusuluhisha mzozo huo.

Mwanasheria mkuu wa serikali Amos Wako ametowa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru juu ya matokeo hayo ya uchaguzi yanayobishiwa.