1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha mashambulio

19 Januari 2015

Kitisho cha kutokea shambulio dhidi ya mwasisi mmojawapo wa Pegida katika maandamano yao huko Dresden chapelekea maandamano kuzuwiliwa katika mji huo wa mashariki ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1EMXg
Polisi ikilinda usalama katika maandamano ya 5.01.2015 ya Pegida huko DresdenPicha: picture-alliance/dpa/A. Burgi

Wafuasi wa vuguvugu la wazalendo wa Ulaya dhidi ya kuenea imani ya dini ya kiislam barani Ulaya na dhidi ya wimbi la wakimbizi nchini Ujerumani, Pegida wamelazimishwa kufutilia mbali maandamano yao ya kila wiki hii leo katika mji wa mashariki wa Dresden kutokana na kitisho cha mashambulio mnamo wakati huu ambapo hofu za kuzuka mashambulio ya kigaidi ya wafuasi wa itikadi kali zimeenea barani Ulaya.

Maandamano ya vuguvugu hilo yataendelea kama kawaida hii leo katika miji kadhaa mengine ya Ujerumani.

Polisi mjini Dresden imetangaza marufuku ya kufanyika maandamano katika mji huo ikitoa sababu za kutokea shambulio la kigaidi.Msemaji wa polisi mjini Dresden Thomas Gleithner amezungumzia fununu walizopokea kutoka idara kuu ya upelelezi ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani na kutoka idara ya upelelezi ya jimbo la Saxony.Fununu hizo zinazungumzia wito uliotolewa kutaka waandalizi wa maandamano ya vuguvugu la Pegida wauliwe.Msemaji wa polisi ya Dresden Thomas Gleithner anasema:"Kuna fununu zaidi kwa mfano kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo imeelezwa kwa kiarabu kwamba Pegida ni adui wa dini ya kiislam.Kuna mtu aliyetajwa kwa jina pia miongoni mwa waandalizi wa maandamano ya Pegida kuwa shabaha ya mashambulio.Lakini kama tujuavyo mashambulio ya kigaidi hayachagui,hayamdhuru mtu mmoja tu,na katika hali hii,yanaweza kuwadhuhuru maelefu,kwa hivyo tunaona hatari ni kubwa."

Hata maoni ya karaha yaachiwe

Vyama vya upinzani katika bunge la shirikisho Bundestag vimekosoa marufuku hayo.Mkuu wa kundi la walinzi wa mazingira Anton Hofreiter amekiambia kituo cha televisheni cha ZDF leo asubuhi,"kuzuwiliwa haki za kimsingi" ni jambo linaloudhi sana."Maandamano ya Pegida ni karaha,hata hivyo maafisa wa serikali wanabidi wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha hata "maoni ya karaha"watu wana uhuru wa kuyatoa.

Protest gegen Demo der Anti-Islam-Bewegung „Kögida in Köln 14.01.2015
Maandamano kupinga vuguvugu la Pegida mjini Cologne,januari 14.mwaka huu wa 2015Picha: picture-alliance/dpa/Henning Kaiser

Katika mjadala wa kwanza na vyombo vya habari,mmojawapo wa waanzilishi wa vuguvugu la Pegida Kathrin Oertel amesema katika kipindi cha "Günther Jauch" cha kituo cha kwanza cha televisheni ARD hawataki kutoka majiani.Wanataka kuendelea kuishinikiza serikali.

Miito ya kujadiliana na serikali inazidi kutolewa

Spika wa zamani wa bunge la shirikisho Wolfgang Thierse wa kutoka chama cha SPD amewataka wafuasi wa vuguvugu la Pegida,watilie maanani yanayofanywa na serikali-kusema serikali haifanyi chochote dhidi ya kitisho cha itikadi kali na wanaotumia vibaya haki za ukimbizi si kweli.

Wolfgang Thierse SPD Vize-Vorsitzender des Bundestages
Wolfgang Thierse wa chama cha SPDPicha: DW/R. Romaniec

Mbunge wa chama cha CDU Jens Spahn anawakosoa kwa upande wake PEGIDA akisema hawataki kutilia maanani hoja za wengine.Ni ujinga kuweka katika wezani mmoja dini ya kiislam na itikadi kali amesisitiza Spahn.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/epd/AFP

Mhariri:Josephat Charo