1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yaendelea Myanmar

25 Septemba 2007

Licha ya onyo kali kutoka utawala wa kijeshi watawa wa Budha waendelea kuongoza maandamano nchini Myanmar kudai demokrasia na uhuru wa kujieleza.

https://p.dw.com/p/CH7n
Watawa Myanmar
Watawa MyanmarPicha: AP

Kiasi cha umati wa waandamanaji laki 1 ukiongozwa tena na watawa wa madhehebu ya Budha,haukujali tena hii leo amri ya utawala wa kijeshi kuacha kuandamana mjini Yangon dhidi ya utawala huo .

Kuna uvumi wanajeshi wamepewa amri kuwafyatulia risasi na magereza yameandaliwa kwa wimbi la kamatakamata.Rais George Bush wa Marekani,atazamiwa leo kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya utawala huo wa kijeshi wa Myanmar.

Licha ya maonyo makali kutoka watawala wa kijeshi watu wasijikusanye kwa maandamano,vikosi vya usalama havikuonekana barabarani mjini Yangon hii leo.

Kiasi cha watawa 30,000 walioongoza umati wa waandamanaji 70.000 hadi kwenye kitovu cha mji mkuu huo na kujikusanya kandoni mwa Pagoda na karibu na Jumba kuu la jiji hilo.

Wakati watawa wakiomba dua na kupaza sauti kandoni mwa pagoda hilo,wafuasi wao walishika kikuza sauti kuhutubia umati uliokuwa hapo.Baadhi ya watawa wakivalia mavazi yao ya rangi nyekundu walishika mabiramu yaliosema:

“Twadai chakula cha kutosha,mavazi na maskani pamoja na suluhu katika taifa.Uhuru kwa wafungwa wote wa kisiasa.”Mtawa mmoja alinukuliwa kusema kwamba, maandamano haya mfululizo sio tu kudai hali bora za wananchi,bali pia kwa watawa kugombea demokrasia na kwa wananchi kujiamulia hatima yao.

Maandamano ya leo ya siku ya 8 mfululizo, yamefanyika licha ya amri iliotolewa kwa viongozi wa dini ya madhehebu ya Budha kukomesha harakati zote za kisiasa na warejee maskani mwao.

Uvumi ukazagaa mjini Yangon leo kuwa wanajeshi yamepewa amri kuwafyatulia risasi waandamanaji na kwamba baadhi ya wanajeshi, wamenyoa vipara kama wafanyavyo watawa ili kujipenyeza miongoni mwao kuzusha fujo ili majeshi ya serikali kuzima maandamano yao ya amani.

Maandamano haya ya sasa nchini Myanmar, zamani Burma,yanalingana moja kwa moja na wimbi la maandamano ya kilio cha demokrasia ya 1988 yaliomalizikia kwa bahari ya damu na vifo vya watu 3,000.

Wimbi la maandamano la wakati ule kama la hivi sasa yamepaliliwa na hali mbaya za kiuchumi na yote yalianza pole pole na kupata nguvu na kuselelea kwa wiki kadhaa.

Darasa moja lakini limepatikana.Watawa wanaoongoza maandamano haya, mara hii wanachukua hadhari ya kuweka nidhamu ili kutoupa utawala wa kijeshi kisingizio cha kuwafyatulia risasi kama walivyofanya miaka 20 iliopita.

Jana,umma wa hadi laki 1 ulimiminika barabarani mjini Yangon,mji mkuu, na kuufanya utawala wa kijeshi kutoa onyo utawachukulia hatua viongozi wa maandamano.Lakini, leo hii umma huo umerudi kuandamana dhidi ya serikali.