1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yaendelea Tunisia

23 Januari 2011

Kiasi waandamanaji 1,000 kutoka maeneo ya vijijini ya Tunisia ya kati, wanaotaka kujiuzulu kwa serikali ya mpito, leo wamewasili kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tunis.

https://p.dw.com/p/101Bn
Rais wa mpito wa Tunisia, Foued Mebazaa (Kulia) na Waziri Mkuu, Mohamed GhannouchiPicha: picture alliance / dpa

Waandamanaji hao kutoka mkoa masikini wa wakulima ambao ndio walichochea maandamano dhidi ya utawala wa kimabavu mwezi uliopita, wanataka kujiuzulu kwa serikali iliyochukua nafasi baada ya kuondolewa madarakani, Zine El Abidine Ben Ali.

Tunesien Unruhen Demonstration Ben Ali Tunis 20.01.2011
Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya mji mkuu wa Tunisia, TunisPicha: picture alliance/dpa

Wakiandamana katikati mwa Tunis, waandamanaji hao wamesema wamekwenda kwenye mji huo kuiondoa madarakani serikali. Maandamano hayo ya ukombozi yalianza jana kwenye mji wa Menzel Bouzaiane, ambako mtu wa kwanza aliuawa katika maandamano ya kupinga utawala wa Ben Ali.

Kumekuwa na maandamano ya kila siku katika siku za hivi karibuni, kutaka kujiuzulu Waziri Mkuu Mohammed Ghannouchi, ambaye amekuwa katika wadhifa huo tangu mwaka 1999 na ameendelea kubakia madarakani, licha ya kuanguka kwa Ben Ali.

Waandamanaji hao pia wanataka kuvunjwa kwa kilichokuwa chama tawala cha RCD, ambacho kilitawala siasa za Tunisia kwa miongo kadhaa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri: Hamidou, Oummilkheir