1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yanaendelea nchini Syria licha ya uamuzi wa kubatilisha sheria ya hali ya hatari

22 Aprili 2011

Mageuzi yaliyotangazwa na rais Bashar al Assad ili kutuliza kilio cha wananchi,hayatoshi wanasema wapinzani.Wanataka wafungwa wa kisiasa waachiliwe huru na utawala wa chama kimoja ukome.

https://p.dw.com/p/112ME
Maandamano nchini SyriaPicha: Picture-Alliance/dpa

Rais Bashar al Assad wa Syria ameamuru kubatilishwa sheria ya hali ya hatari iliyokuwa ikitumika tangu miaka 50 iliyopita nchini humo. Kwa mujibu wa televisheni ya taifa, rais Assad ametangaza kanuni mbili; ya kwanza kuhusu kuvunjwa mahakama ya usalama wa taifa na ya pili kuruhusu haki ya wananchi kuandamana kwa amani. Wapinzani wanahofia lakini kwamba licha ya kubatilishwa sheria ya hali ya hatari, maandamano yanayofanyika hivi sasa nchini humo, yataendelea kukandamizwa. Wapinzani wameshasema uamuzi huo hautoshi, wanataka ukome utawala wa chama kimoja -Baath.

Msalaba juu ya kanisa na kati ya miezi miwili michanga kuna minara miwili juu ya msikiti. Hicho ndio kitambulisho kinachotumiwa na kundi la tovuti ya Facebook linalojiita "Mapinduzi ya Syria 2011" kuwataka wananchi wateremke majiani mnamo siku ya leo ya Ijumaa kuu kuandamana kote nchini Syria. Asili mia 15 ya Wasyria ni wakristo."Moyo mmoja, mkono mmoja na lengo moja"-hiyo ndio kauli mbiu ya maandamano ya leo ya kudai uhuru zaidi. Kwa wakati wote ambao vikosi vya usalama vitaeandelea kufanya wakitakacho, kwa wakati wote ambao mahakama haitakawa huru, upande wa upinzani hautatosheka na uamuzi wa kubatilisha sheria ya hali ya hatari, miaka 50 tangu ilipoanza kutumika, kama alivyotangaza rais Baschar al Assad:

"Kuna wanaodai kubatilishwa sheria ya hali ya hatari ni hatari kwa usalama wetu. Mie lakini nna maoni tofauti na hayo. Nnahisi kwa namna hiyo tunahakikisha na kudhamini hadhi na muruwa wa wananchi."

Syrien Präsident Bashar Assad hält eine Rede vor seinem Kabinett in Damaskus
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: dapd

Matamshi hayo hayalingani hata kidogo na ukweli wa mambo. Shirika linalopigania haki za binaadam Amnesty International linasema watu 220 wameuwawa tangu machafuko yalipoanza huko Syriwm. Na leo pia maandamano yamepangwa kuitishwa Deraa, Homs na kwengineko. Vikosi vya usalama vimeshawekwa tayari katika kila pembe ya nchi hiyo.

Upande wa upinzani unahisi hatua zote zinazochukuliwa mfano kumuachisha kazi gavana wa Homs na kumteuwa mwengine ni njama tuu za kutaka kudhoofisha maandamano. Wanataka waafungwa wote waliokamatwa kuambatana na sheria ya hali ya hatari waachiliwe huru na watu waachiwe waandamane bila ya kulazimika kuomba ruhusa serikalini.

Beerdigung des Soldaten Munir Al-Jallad in Syrien
Maziko ya mwanajeshi mmoja aliyeuwawa nchini SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Syria inawatuhumu wageni kuwa ndio wanaoyaandaa machafuko nchini humo. Inadai lengo ni kuchochea mivutano ya kikabila. Ukweli lakini ni mwengine kabisa: Wasyria wote, kutoka tabaka zote za jamii, imani zote za kidini na makabila yote wanashiriki katika maandamano hayo.

Mwandishi:Leidholdt Ulrich/Amman WDR/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Josephat Charo