1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yazuka upya Misri

19 Juni 2012

Maandamano makubwa yanapangwa kufanyika katika mjini Cairo, dhidi ya uamuzi wa Baraza la Kijeshi kujitwalia madaraka yote, huku Marekani na Ujerumani zikilitaka Baraza hilo lirejeshe madaraka kwa utawala wa raia.

https://p.dw.com/p/15HZo
Wafuasi wa Mohammed Mursi wa Udugu wa Kiislamu wakifurahia ushindi wa mgombea wao.
Wafuasi wa Mohammed Mursi wa Udugu wa Kiislamu wakifurahia ushindi wa mgombea wao.Picha: picture-alliance/dpa

Maandamano ya leo (19 Juni 2012) yameitishwa na makundi kadhaa yaliyoshiriki mapinduzi ya Februari 2011, baada ya wanajeshi kujitwalia nguvu za bunge kufuatia uamuzi wa mahakama wa wiki iliyopita kulifuta bunge lililokuwa likitawaliwa na vyama vyenye mtazamo wa kidini.

Waandamanaji wamekasirishwa na tangazo la jana la Baraza la Kijeshi, ambalo pamoja mengine lilijipa uwezo wa kuvipigia kura ya veto vifungu katika katiba yoyote mpya ijayo. Waandamanaji hao wanasema mapinduzi yao ya Februari 2011 tayari yameshapinduliwa na wanajeshi, na sasa wako tayari kufanya mapinduzi mengine.

"Watu wamechanganyikiwa na kuchoka sana. Tumetumia muda wa mwaka mmoja na nusu mitaani kupigania uhuru wetu na haki za kiraia. Lakini hatujafanikiwa kupata chochote." Anasema Shady Abdullah, mmoja wa waandamanaji hao.

Mkanganyiko kweye matokeo ya uchaguzi wa rais

Tangazo la Baraza la Kijeshi kujitwalia madaraka limekuja pia katika wakati ambapo matokeo ya uchaguzi wa raisi yanabishaniwa kati ya mgombea wa Chama cha Udugu wa Kiislamu, Mohammed Mursi, na mshindani wake, waziri mkuu wa zamani Ahmed Shafiq. Kila upande kati yao, unadai kushinda uchaguzi wa mwishoni mwa juma.

Mohammed Mursi wa Udugu wa Kiislamu.
Mohammed Mursi wa Udugu wa Kiislamu.Picha: dapd

Gazeti la serikali la Al-Ahram limesema kupitia mtandao wake kuwa baada ya kura za majimbo 27 kuhisabiwa, Mursi anaongoza kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Shafiq. Sherehe za ushindi zimeripotiwa kwenye makao makuu ya Udugu wa Kiislamu, ambako Mursi amewashukuru wapiga kura na kuahidi kufanya kazi na Wamisri wote bila kujali dini zao.

Hata hivyo, meneja wa kampeni za Shafiq, Ahmed Sarhan, ameliita tangazo hilo kuwa limetokana na takwimu za uongo na kudai kuwa ni Shafiq ndiye anayeongoza kwa kati ya asilimia 51 na 52 hadi sasa.

Marekani na Ujerumani zalionya Baraza la Kijeshi

Wakati hayo yakiendelea, Marekani imelitolea onyo Baraza la Kijeshi la Misri kwamba uhusiano kati ya mataifa hayo mawili utategemea na namna Baraza hilo litakavyokubali kurejesha utawala wa kiraia kwa raisi aliyechaguliwa na Wamisri na msaada wa mabilioni ya dola kwa Misri utaathirika moja kwa moja.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.Picha: dapd

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Victoria Nuland, amesema nchi yake inatiwa wasiwasi sana na hatua ya Baraza la Kijeshi kurefusha muda wa kuwapo madarakani na amelitaka Baraza hilo kurejesha imani ya kimataifa kwa kutimiza ahadi zake.

Kauli kama hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, aliyetaka kurudishwa kwa utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo.

"Tunatarajia Baraza Kuu la Kijeshi litakabidhi madaraka kwa raia waliochaguliwa kidemokrasia. Hili inajumuisha bunge, ambalo litawezeshwa kufanya kazi haraka iwezekanavyo. Na kwamba pia Baraza hilo litafuata utaratibu wa kisiasa ambapo taasisi zote za kidemokrasia zitakuwa na imani na Misri." Amesema Westerwelle.

Kwa vyovyote kinachoshuhudiwa sasa nchini Misri ni mapambano ya madaraka kati ya Baraza la Kijeshi na Udugu wa Kiislamu. Ambapo Baraza la Kijeshi limetangaza kujitwalia nguvu zote za bunge, Udugu wa Kiislamu umesema kwamba bunge hilo lililovunjwa na Mahakama ya Katiba bado ni halali na kwamba unashiriki kwenye maandamano yanayoanza leo dhidi ya kile walichokiita "mapinduzi ya kijeshi dhidi ya mapinduzi ya umma".

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman