1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maduka, na Magari yateketezwa

Eric Kalume Ponda8 Desemba 2008

Kwa siku ya tatu mfululizo, ghasia ziliendelea kukumba miji kadhaa nchini Ugiriki, huku mamia ya waandamanaji wakipambana na maafisa wa usalama na kuharibu mali.

https://p.dw.com/p/GBUr
Waandamanaji mjini Athens,Ugiriki wakiteketeza mali kupinga mauaji ya kijana wa miaka 15.Picha: AP


Maandamano hayo yaliyoanza siku ya jumamosi, yameitishwa na makundi ya kutetea haki za binadamu,kufuatia kuuawa kwa kijana mmoja wa miaka 15, aliyepigwa risasi na maafisa wa Usalama mjini Athens siku ya Jumamosi.

Zaidi ya waandamanaji 2,000 wanaoshiriki maandamano hayo yaliyoitishwa kote nchini humo kupinga mauaji ya kijana huyo ,wamevunja na kuteketeza maduka na benki ikiwemo benki ya taifa mjini Salonika, kupinga mauaji ya kijana huyo.

Maandamano hayo sasa yamesamba katika zaidi ya miji mitano mikubwa nchini humo huku waandamanaji hao wakifunga barabara zinazoelekea chuo kikuu mjini Athens.

Polisi wanasema kuwa zaidi ya watu 14 wamekamatwa huku waalimu na chama cha kisiasa kinachozingatia sera kali za mrengo wa kushoto cha KKE, kikitisha kuunga mkono maandamano hayo.

Chama hicho cha kikoministi kinatarajiwa kuitisha mkutano wake wa kwanza kuhusiana na suala hilo katika eneo la Omonia mjini Athens.

Maafisa wa usalama walionekana kuzidiwa nguvu na waandamanaji hao, ambao sasa wamethibiti barabara za miji mikubwa nchini humo, baada ya kuvunja ofisi za serikali pamoja na ofisi za baraza kuu la Mji wa Salonika.

Kijana huyo Andreas Grigoropoulos,aliyekuwa miongoni mwa kundi la vijana 30, aliuawa usiku wa jumamosi,baada vijana hao kurushia mawe gari la maafisa wa usalama waliokuwa wakishika doria katika barabara za mji mkuu Athens.

Yadaiwa mmoja wa maafisa hao alitoka nje ya gari hilo na kumpiga risasi tatu kifuani kijana huyo, na kufariki njiani akipelekwa hopitalini.

Mamia ya waanadamanaji hao, hasa vijana waliojifunika nyuso wamekuwa wakikabiliana na maafisa wa usalama kwa kuwarushia mawe na mabomu ya petroli maafisa wa usalama.


Kwa mujibu wa ripoti kutoka mjini Athens, zaidi ya magari 20 yameteketezwa, huku benki 17 zikivunjwa na maduka kuporwa na waandamanaji hao katika mji wa Solaniika ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Ugiriki.


Waziri wa mashauri ya ndani nchini humo Prokopis Pavlopoulos aliwaambia wandishi wa habari kwamba tayari afisa mkuu wa Polisi wa kituo kilichoko karibu na mahala alipouawa kijana huyo pamoja na maafisa wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo, wamesimamishwa kazi huku uchunguzi ukianzishwa.


Hata hivyo waandamanaji hao wamesema wataendelea na maandamano yao hadi pale haki itakapotekelezwa na maafisa hao kufikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka.


Kisa hiki kimezua kumbukumbu ya mauaji ya kijana mwengine wa umri wa miaka 15 Michalis Kaltezas aliuawa na Polisi mwaka wa 1985 na kupelekea maandamano makubwa katika baadhi ya miji mikubwa ya nchi hiyo.