1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya hali ya hewa yageuza mienendo ya dunia

Josephat Charo27 Desemba 2007

Mabadiliko ya hali hewa yanaipundua miungano ya kimataifa

https://p.dw.com/p/Cgb9
Utoaji wa gesi za viwandani unalaumiwa kwa kusababisha mabadiliko ya hali ya hewaPicha: AP

Kwa mara nyingine tena binadamu anakabiliwa na hatari ya kutokea janga kubwa. Kitisho cha maangamizo kutokana na makombora ya nyuklia yanaoweza kuvurumishwa kwa kubonyeza kifungo kimoja tu kimetoa mwanya kwa uwezekano sumbufu wa mabadiliko ya hali ya hewa kufikia kiwango kisichoweza kurudi nyuma. Na hali hii inapindua utamaduni wa miungano ya kimatiafa na mawazo ya kisiasa.

Ingawa kitisho kinachomkabili binadamu kimeshatambuliwa kwa matamshi mengi ya kidiplomasia, dola kuu duniani hazilipi uzito unaotakikana tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Migawanyiko ya zamani na mizozo inayotokana na maswala ya kiuchumi, kibiashara na nadharia mbalimbali, inaendelea kutawala.

Brazil kwa mfano inatakiwa kujiunga na Umoja wa Ulaya katika ushirikiano unaolezwa kuwa wa kiadilifu na kidhamana, na kujiepusha mbali na China, nchi mbayo hivi sasa inatoa kiwango kikubwa cha gesi za viwandani na iliyo na tabia ya kutojali linapokuja swala la hali ya hewa. Hayo yamesemwa na profesa wa ushirikiano wa kimataifa, Eduardo Viola, wa chuo kikuu cha Brasilia nchini Brazil.

Kwa mtazamo wake profesa Viola anaona ushirikiano kati ya nchi zinazotoa viwango vikubwa vya gesi za viwandani unaweza kuunda kanuni zinazohitajika kuzuia mabadiliko hatari ya hali ya hewa, ambayo yatatokea iwapo kiwango cha joto ardhini kitapanda kwa zaidi ya nyuzi mbili katika karne hii. Hali itakayosaidia kuleta matokeo ni ikiwa wapigaji kura wa Marekani watamchagua rais mpya mnamo mwezi Novemba mwaka ujao wa 2008 atakayeweza kuongoza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali hewa duniani.

Brazil ni nchi ya sita katika orodha ya mataifa yanayotoa viwango vikubwa vya gesi za viwandani baada ya China, Marekani, Umoja wa Ulaya, India na Urusi. Profesa Eduardo Viola anasema Brazil inaweza kuchangia katika juhudi hizo kwa kuungana na serikali za Umoja wa Ulaya na Japan kushirikiana katika mpango wa kuleta mabadiliko katika uchumi yatakayohakikisha viwango vya gesi ya carbon dioxide vinapungua. Aidha profesa Viola amesema Brazil inaweza kulifanikisha hilo kwa kujitolea kwa dhati kuyatimiza majukumu makubwa na kuchukua tena usukani katika kuongoza juhudi za kimazingira kama ilivyofanya katika miaka ya 1990.

Ukweli unaoshangaza kwamba ukataji wa miti ndio unaochangia asilimia 60 ya utoaji wa gesi za viwandani nchini Brazil una maana kwamba nchi hiyo inaweza kupunguza utoaji wa gesi hizo kwa gharama ndogo ikilinganishwa na nchi nyingine zinazotoa viwango vikubwa vya gesi hizo.

Brazil ilitoa tani bilioni moja za gesi ya carbon dioxide mnamo mwaka wa 2004 lakini tayari kiwango hicho kimepungua kwa zaidi ya asilimia 30 kwa sababu kasi ya ukataji wa msitu wa Amazon imepungua kwa zaidi ya asilimia 50 katika miaka mitatu iliyopita. Hata hivyo kauli ya kutatanisha ya rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, inaizuia nchi hiyo kutumia ufanisi huo kuimarisha nafasi yake katika mazungumzo kuhusu hali ya hewa, amelalamika Rubens Born, mratibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Vitae Civilis. Aidha mratibu huyo amesema ikiwa Brazil ingekuwa huru kutoka kwa kundi la nchi 77, G77, pamoja na China, ingeweza kuibadili hali ya baadaye ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Kundi la G77 lililo na nchi 130, liliundwa mnamo mwaka wa 1964 kuyalinda masilahi ya pamoja ya kiuchumi ya nchi zinazoendelea. Lakini kundi hilo halifanyi kazi yoyote kuhusu maswala ya hali ya hewa kwa sababu ya kuwepo China na nchi zinazosafirisha mafuta ya petroli, ambazo zina maslahi yanayopingana na nchi nyingine wanachama wa kundi hilo.

Rubens Born amesema alivunjwa moyo na mkutano kuhusu mabadiliko ya hewa uliofanyika kati ya tarehe 3 na 15 mwezi huu katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia. Kuna ufanisi fulani uliopatikana katika mkutano huo, lakini anasema hautoshi kuhakikisha mazungumzo yanaendelea kwa kasi inayotakikana huku makubaliano yakitakiwa yafikiwe katika kipindi cha miaka miwili ijayo.