1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya tabianchi na sera zawatatiza wakulima Malawi

15 Agosti 2017

Hali ya mabadiliko ya tabianchi na sera zilizopo nchini Malawi zinawachangaya wakulima kuchagua mbegu kwa ajili ya kilimo, jambo ambalo ni changamoto kubwa katika shughuli zao za kila siku.

https://p.dw.com/p/2iDhI
Malawi Forscherin Seline Meijer
Wakulima wanawake nchini MalawiPicha: Seline Meijer

Elias Kanyangale, mmoja wa wakulima wa Malawi anafurahia mavuno mazuri ya mahindi yake, hali iliyochangiwa na mvua kubwa mwaka huu. Kanyangale, mwenye umri wa miaka 44, kutoka kijiji cha Kalumbu, anasema tani tano za mahindi hayo ni mara mbili ya mavuno ya mwaka uliopita, na pia amepanda maharagwe meupe ya soya.

Lakini ana wasiwasi kuhusu pato lake kwa sababu anahisi huenda labda asipate bei nzuri ya mazao yake sokoni. Hali ya mabadiliko ya tabianchi na sera zilizopo nchini humo zikiwa changamoto kuu.

Wakulima wengi wadogo wa mahindi nchini Malawi wamepanua kilimo chao na kujihusisha na kilimo cha maharagwe meupe ya soya na njugu wakitarajia bei nzuri sokoni endapo zao moja litaathiriwa na ukame.

Kutokana na changamoto zinazowakabili, wakulima wengi wanatatizika kuchagua mbegu za kupanda na muda wa kupanda.

Hali ya hewa mwaka jana iliyosababisha mafuriko na ukame, imewaacha wengi wakikabiliwa na uhaba wa chakula.

Baadhi ya wakulima waliofuata muongozo wa wataalamu wa kubadilisha kilimo, wamepanda tumbaku na maharagwe meupe ya soya mwaka wa 2016 kulingana na matarajio ya bei za kuvutia mwaka huu.

Lakini hali ya kuwa na mazao mengi kupita kiasi sokoni, imewavunja moyo na kuwazuia kupata soko la mazao yao ya ziada ya maharagwe meupe aina ya soya.

Huku wale waliopuuza muongozo huo na kusalia na kilimo cha mahindi, wakijipata pabaya kutokana na marufuku iliyowekwa na serikali dhidi ya usafirishaji nje wa mahindi yaliokuzwa kwa matumizi ya nyumbani.

Kuwasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko

Shirika moja nchini Malawi limekuwa likiwasaidia wakulima wadogo kubadilisha kilimo chao na kuwacha kutegemea zao moja kwa kwa kuwapa mafunzo ya mbinu bora za kilimo biashara.

Mkulima akiendelea na shughuli zake shambani
Mkulima akiendelea na shughuli zake shambaniPicha: DW/C. Mavhunga

Peter Kaupa, mmoja wa afisa kutoka muungano wa wakulima wadogo nchini Malawi, NASFAM, anaelezea kwa kusema, "kubadilisha mbinu za kilimo haitokei mara moja na mwaka huu wakulima watapanda zaidi tumbaku kwasababu ya bei nzuri na huenda watapunguza kupanda maharagwe meupe ya Soya kwasababu ya msimu huu."

Anasema "wakulima waliozowea kilimo cha aina moja wanasita kubadilisha mazowea yao na kung'ang'ania kuishia kufanya maamuzi ya haraka wanapokabiliwa na hali ya mabadiliko ya tabia nchi na athari za sera kutoka serikali kuhusu mauzo ya mimea na usafirishaji nje wa bidhaa."

Zaidi ya wakulima wadogo elfu hamsini kutoka maeneo bunge matano nchini Malawi watafunzwa jinsi ya kupata taarifa kuhusu mabadiliko ya nchi, kupata bima inayozingatia hali ya hewa na matumizi ya aina tofauti ya mbegu zinazostahamili ukame.

Alice Kachere, ambaye pia ni mkulima wa mahindi jijini Lilongwe aliyepanda mahindi mengi kuliko maharagwe meupe ya soya mwaka huu, akihofia bei ya chini ya zao hilo, anatarajia kuuza mahindi yake ya zaidi ya tani 12 na kununua mbegu na vifaa atakavyotumia msimu ujao.

Mwaka jana alipanda tumbaku lakini akapata hasara kubwa, hali iliyompeleka kukopesha pesa ili kujiandaa kwa msimu huu. Ana hamu kubwa ya kukamilika kwa marufuku iliyopo ili apate kutumia nafasi nzuri ya kibishara na taifa la Kenya.

Mwezi Mei waziri wa biashara wa Malawi Joseph Mwanamvekha amesema serikali ipo tayari kutoa leseni za kuwaruhusu wafanyibiashara kuuza bidhaa zao nje iwapo wataweza kuonyesha kuwa walinunua mahindi kwajili hiyo na kwa wakulima ambao wamepanda mahindi haswa kwajili ya kuuza bidhaa nje ya nchi.

Serikali bado haijaweka bayana lini itaondoa marufuku dhidi ya mahindi ya kutumika nyumbani lakini ngojangoja hiyo inaumiza matumbo ya wakulima wanaotarajia mapato bora kutokana na mauzo ya mahindi.

Malawi inakadiria mavuno yatani ya zaidi millioni tatu ya mahindi mwaka huu, ambayo ni ongezeko la thuluthi ya uzalishaji wa mahindi katika mwaka wa 2015/16.

Kukiwa na utabiri wa mvua ya el Nino mwaka huu, kulingana na mkuu wa taasisi ya ushirikano wa umoja wa Ulaya nchini Malawi, Lluis Navarro, wakulima watafanikiwa iwapo watajiandaa kwa msimu wa ukame kwa kujihusisha na kilimo mbadala na kuchagua aina za mbegu zinazoweza kuhimili ukame.

Taasisi hiyo imekuwa ikiwekeza katika kilimo cha taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Mwandishi: Fathiya Omar/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef